Breaking News

Maombi ya Lissu kufikishwa mahakamani yapangiwa jaji


Kwa ufupi

Pamoja na kupangiwa jaji lakini hadi sasa bado haijajulikana ni lini kesi hiyo itaanza kusikilizwa kama ni leo au siku nyingine.

Wakati Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akiendelea kushikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi, maombi yaliyofunguliwa na mawakili wanaomwakilisha, wakiongozwa na Fatma Karume, yamepangiwa jaji wa kuyasikiliza.

Maombi hayo yaliyofunguliwa Mahakama Kuu Dar es Salaam, Ijumaa iliyopita ya kuomba mahakama iiamuru Serikali, imfikishe mahakamani Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Mwanasheria Mkuu wa Chadema.

Maombi hayo yaliyofunguliwa chini ya hati ya dharura yamepangwa kusikilizwa na Jaji Ama-Isario Munisi.

 

Hata hivyo habari kutoka masjala ya jinai ya Mahakama Kuu zinasema kuwa bado maombi hayo hayajapangiwa tarehe ya kusikilizwa kwa kuwa hadi sasa jalada hilo liko kwa Jaji Munisi.

 

Hadi sasa haijajulikana kama maombi hayo yatasikilizwa leo au lini.

 

Mawakili hao wa Lissu walifikia uamuzi wa kufungua maombi hayo baada ya polisi kumshikilia kwa muda mrefu bila kumfikisha mahakamani.

 

Lissu alikamatwa na polisi tangu Alhamisi ya juma lililopita, wakati akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kusafiri kuelekea Rwanda kuhudhuria mkutano wa vyama vya wanasheria Afrika.

No comments