Breaking News

RPC Shana: Majambazi Nane Yakamatwa Pwani


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
JESHI la polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watu nane wanaosadikiwa kuwa majambazi kwa tuhuma za kuhusika na tukio la utekaji wa gari.
 
Aidha jeshi hilo limefanikiwa kuwatia mbaroni wahamiaji haramu saba kutoka nchi ya Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
 
Tukio hilo lilitokea Juni 4 mwaka huu, katika eneo la Vigwaza ambapo watu wawili waliojifanya wasamaria wema walisimamisha gari hiyo yenye namba za usajili T 311 DHS aina ya Fuso lililokuwa likiendeshwa na Abeid Victor likitokea Dar es Salam kwenda Iringa.
 
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani (ACP) Jonathan Shanna alithibitisha kutokea kwa tukio hilo .
 
Alieleza watu hao wawili walimsimamisha dereva huyo wakihitaji msaada lakini baadae walimgeuka na kumpora gari hilo.
 
Shanna alisema, gari hilo lilikua limebeba unga wa ngano kilo 205, baada ya tukio hilo Jeshi hilo kwa kushirikiana na polisi wa mkoa wa Morogoro waliendesha msako ambao ulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao kwenye mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Dar es Salam.
 
“Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na mzigo huo wa unga na vifaa mbalimbali vya gari hilo waliloliteka”
 
“Baada ya kuhojiwa walikiri kuhusika katika tukio hilo na kisha kuonyesha walipohifadhi mzigo huo na vifaa vya gari vilivyokua vimekatwa ambavyo ni kichwa cha gari, kadi ya gari, namba za usajili wa gari, giabox na engine” alisema.
 
Shanna aliwataja watuhumiwa hao ni pamoja na Juma Chilala, Edgar Musa, Abdallah Mohamed, Ashama Bakari, Said Selemani, Kassim Nassoro na Masumbuko Selemani .
Alisema anatarajia kufikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.
 
Katika tukio lingine Jeshi hilo limefanikiwa kuwatia mbaroni wahamiaji haramu .
 
Wahamiaji hao walikamatwa katika msako unaoendeshwa na Jeshi hilo katika eneo la wilaya ya Kipolisi ya Chalinze ambapo raia hao wa Ethiopia walikutwa kwenye nyumba ambayo haijakamilika huko Pingo.
 
Shanna aliwataja wahamiaji hao kutoka Ethiopia kuwa ni Malakwi Abala(20),Elias Tadela(40), Mohamed Awole(31), Degafa Hanadamo(22)Sadebo Cakebo(38),Abraham Lamango(35) na Mahalu Tahifae wote watakabidhiwa kwa idara ya Uhamiaji kwa taratibu za kisheria.
 
Aliwaonya wahamiaji ambao wanaingia nchini bila kibali na yeyote atakayekamatwa  Sheria itachukua mkondo wake.

No comments