Breaking News

Mtoto wa miaka 11, adaiwa kubakwa, kunyongwa

Baba wa marehemu Jimmy Marealle mama wa marehemu Agnes Msigala, wakizungumza kuhusu kifo cha mtoto wao  Nora, kwenye msiba unaofanyika Sinza Mori jijini Dar es Salaam.  Picha  na Beatrice Moses. 

Kwa ufupi

Mmoja wa wajomba wa mtoto aliyefariki anashikiliwa  na polisi wa Kituo cha Mabatini kwa ajili ya mahojiano.

By Beatrice Moses,Mwananchi bmoses@mwananchi.co.tz

Mtoto wa miaka 11 (jina tunalo) amekutwa amekufa katika mazingira ya kutatanisha huku kukiwa na madai kwamba alibakwa kisha akanyongwa. 

Mtoto huyo ni wa pekee kwa wazazi wake na ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Atlas ya jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa wanafamilia hiyo, mwili wa mtoto huyo ulikutwa ukiwa umepiga magoti huku shingo yake ikining'inia kwenye kitanzi kinachodaiwa kiliwekwa kama mtego wa kumkamata paka.

Mama wa marehemu Agnes Msigala, akisimulia tukio hilo amesema wakati hayo yanatokea, hakuwepo nyumbani na kwamba bado hawajapewa taarifa rasmi za vipimo.

"Nilipelekwa wodini kumuona mwanangu, nikamwangalia usoni kweli ni Nora, kuna nesi aliniambia wanahisi alibakwa kutokana na jinsi sehemu zake za siri zilivyokuwa, alimfunua kutaka kunionyesha sikuweza kuendelea kumwangalia,” anasema na kuongeza:

"Awali nilipigiwa simu kwamba mwanangu ameanguka, nilipofika pale hospitali Palestina nikachanganyikiwa baada ya kuambiwa nijikaze mwanangu ameshakufa, yupo wodini ndipo nikaenda kumwona.”

Amesema alipoondoka nyumbani asubuhi ya siku ya tukio alimwacha mwanawe akiwa mzima wa afya, akiwa na wajomba zake wawili.

"Nimeambiwa wakati wa tukio walibaki wawili, mdogo wangu wa kiume ambaye tumezaliwa tumbo moja na ndiye kitinda mimba wetu ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi pamoja na yule msichana," amesema.

Amesema mdogo wake huyo wa kiume ni mhitimu wa Chuo cha Uhasibu Arusha na ameajiriwa kwenye Saccos moja jijini hapa.

Baba mzazi wa marehemu Jimmy Mareale amesema kitendo hicho kimemsononesha, hasa kutokana na utata uliojitokeza.

"Sina cha kueleza zaidi ila nimemwambia hadi mke wangu kwamba tuache vyombo husika vifanye kazi sheria ichukue mkondo wake hata ikibainika ndugu wanahusika, nahitaji kujua nini kimemuua mwanangu, "amesema.

Mmoja wa wajomba wa Norah, amesema alienda msibani Kigamboni, lakini akiwa huko alipewa taarifa za msiba huo.

"Hapa inadaiwa alijinyonga mimi ndiye nilifunga kitanzi cha kamba ya manila ili kumnyongea paka ambaye ni msumbufu, juzi alikula mboga,’’ amesema mjomba huyo (jina tunalo).

Habari zilizotufikia zinaeleza kuwa mjomba huyo naye alichukuliwa na polisi muda mchache akiwa msibani hapo, kisha kupelekwa Kituo cha Polisi Mabatini Kijitonyama.

No comments