JINSI YA KUCHAGUA DAWA NZURI KWA KIKOHOZI NA MAFUA
Kikohozi na mafua ni miongoni mwa matatizo ya kiafya ambayo yapo kila siku katika jamii yetu. Hakuna siku hata moja ambayo hospitali au famasi itakosa mgonjwa wa kikohozi au mafua. Wengi wa wagonjwa wa matatizo haya hufika na kuelezea matatizo yao kisha kushauriwa dawa za kutumia na madaktari au wafamasia. Wengine hufika famasi wenyewe na kusema wanataka dawa fulani. Kwa mfano wengi sana hufika famasi na kusema wanataka dawa za mafua za chenga chenga (Nyakati nyingine huwa nacheka na kujiuliza kama wanadhani chenga chenga ndo zinatibu vizuri mafua au hudhani kwamba dawa hizo husaidia kutibu mafua ya aina zote)
Sasa ni njia gani nzuri ya kuchagua dawa za kikohozi na mafua?
VITU VINAVYOSABABISHA KIKOHOZI
Kikohozi ni sehemu ya kinga ya mwili kukabiliana dhidi ya vitu vigeni na vijidudu vya magonjwa katika njia ya hewa. Tunakohoa ili kuondoa vitu hivyo viende nje ya mwili.
Miongoni mwa vitu vinavyoweza kusababisha kikohozi ni pamoja na
Maambukizi ya vijidudu vya magonjwa kama vile bakteria, virusi, minyoo nkUwepo wa vitu vigeni au punje katika njia ya hewaAthari ya baadhi ya dawa (Mfano ni Captopril inayotumika kutibu shinikizo kubwa la damu/presha)Kupaliwa na maji, chakula au hewaMzio (Aleji) kutokana baadhi ya vitu kama vile vumbi
VITU VINAVYOSABABISHA MAFUA
Mafua hutokana na kuzalishwa kwa wingi zaidi kwa ute (mucus) katika sehemu za juu za mfumo wa upumuaji(puani). Yanaweza kuwa mengi zaidi na mepesi kiasi cha kuweza kutiririka au kuwa machache na mazito kiasi cha kuweza kuziba pua.
Miongoni mwa vitu vinavyoweza kusababisha mafua ni pamoja na
Maambukizi ya vijidudu vya magonjwa hususan virusi (Virusi vya mafua)Mabadiliko ya hali ya hewa na kuwa na baridi au unyevu zaidiMzio (Aleji) kutokana na baadhi ya vitu kama vile vumbi, vipodozi, rangi nkUlaji wa pilipili nyingi
JINSI YA KUCHAGUA DAWA
Hakuna dawa moja ambayo inafaa kwa mafua na vikohozi aina zote au vinavyotokana na sababu mbalimbali. Kitu kizuri zaidi kufanya ni kujua chanzo cha mafua au kikohozi chako na kisha kutumia dawa inayofaa zaidi kwa mafua au kikohozi hicho. Njia rahisi zaidi ya kufanya hivyo na kufanikiwa vizuri ni kujieleza vizuri kwa daktari au mfamasia kisha atakushauri dawa nzuri zaidi kwako. Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya kikohozi au mafua na matatizo mengine ambayo unaweza ukawa huyajui, kwa hiyo ni bora kumuelezea daktari au mfamasia jinsi unavyojisikia na kumuelezea chanzo cha tatizo lako (kama hukumbuki mwambie hukumbuki sababu au chanzo chake) ili yeye atafakari zaidi na kukushauri vizuri.
Dawa kama vile Piriton, Cetirizine na Loratadine ni mahsusi kabisa kwa ajili ya mafua au kikohozi kinachotokana na mzio (aleji) tu. Na si vinginevyo.
Virusi vya mafua na kikohozi havihitaji dawa na hata ukitumia dawa huwezi kuviua wala kuvifanya chochote. Na mara nyingi mafua husababishwa na virusi hivyo, kadhalika na kikohozi. Usitumie dawa za kuua bakteria kwa wadudu hawa maana hazitawafanya chochote na wewe utapoteza muda na hela zako pamoja na kuharibu dawa hizo.
Dawa kama vile Amoksilini, Ampisilini, Ampikloksi, Pen V nk ni kwa ajili ya kutibu magonjwa yatokanayo na bakteria tu. Na si kwa matatizo mengine. Hapa naomba tukazie sana maana watu wengi sana hukosea kwa kununua dawa hizi tu kila mara wanapokuwa na kikohozi. Tafadhali pata ushauri wa daktari kwanza kabla ya kuanza kutumia dawa hizi na nyingine zote ambazo ni mahususi kabisa kwa ajili ya maambukizi ya bakteria.
Dawa za maji na vidonge kama vile Coldril, Mucolyn, Koflyn, Cold Cap, Zecuf, Benylin, Good morning, Cofta, Brozen nk ndizo mahususi kabisa kwa ajili ya kikohozi na mafua. Hata hivyo nyingi kati ya dawa hizo zina mchanganyiko wa dawa zaidi ya moja na hufaa kwa aina tofauti za kikohozi au mafua. Pata ushauri kutoka kwa daktari au mfamasia kujua dawa gani ni nzuri sana kwa kikohozi au mafua aina yako. Kama ni mafua yanayochuruzika, mafua yaliyoziba pua, kikohozi kikavu, kikohozi kinachotoa makohozi, ukikohoa kooni panauma na kadhalika.
VIPI USIPOPATA DAWA SAHIHI?
Kikohozi na mafua ya kawaida huwa na uwezo wa kupona yenyewe bila dawa yoyote ndani ya wiki moja tu. Kwa hiyo unaweza kupona kikohozi au mafua bila kula dawa yoyote endapo utajiepusha na vitu vilivyokusababishia kikohozi au mafua hayo.
Tunakunywa dawa kwa malengo makuu mawili tu
Kusaidia kutibu maambukizi ambayo ni lazima dawa itumikeKuwahi kupona na kuondokana na matatizo yanayoletwa na kikohozi na mafua
Kwa hiyo usipotumia dawa sahihi utachelewa kupona tu na hatimaye mafua au kikohozi chako kitapona chenyewe ndani ya hiyo wiki au na siku chache sana.
KUKOHOA KWA MUDA MREFU
Kukohoa kwa zaidi ya wiki mbili huweza kusababishwa na mazingira duni yanayochangia kikohozi mara kwa mara (kwa mfano kupikia jiko la kuni na kuishi kwenye nyumba yenye vumbi na moshi kila siku), maambukizi ya bakteria kama vile wale wanaosababisha kifua kikuu (TB) au matatizo mengine ya ndani ya mwili. Endapo utakohoa kwa muda mrefu (Zaidi ya wiki mbili) basi ni vyema ukaenda hospitali kwa ajili ya uchunguzi, ushauri na matibabu.
Kama bibi au babu au baba au mama wa kijijini wanakohoa kwa muda mrefu basi ni vyema kuwarekebishia makazi na mazingira yao na kuwasaidia matibabu mazuri.
DAWA ZA ASILI
Kabla ya kuja kwa dawa za kisasa kulikuwa na dawa nyingi tu za asili ambazo zilisaidia kutibu magonjwa yetu kadha wa kadha. Kwa upande wa kikohozi na mafua nako ni hivyo hivyo kuna dawa nyingi za asili na nyingine ni za kisasa lakini zimetokana na mimea hii hii tunayoiacha huku kwenye makazi na mashamba yetu.
Mifano ya dawa za asili kwa ajili ya kikohozi na mafua ni Asali na Tangawizi. Mifano ya dawa za kisasa zilizotengenezwa kwa mimea ni Zecuf na Travisil.
MAMBO YA KUZINGATIA
Elimu haina umuhimu mpaka pale itakapotumika. Hakikisha kuanzia sasa na kuendelea unajieleza tu kwa daktari au mfamasia kisha yeye akusaidie kukushauri dawa nzuri zaidi kwa ajili ya ugonjwa wako. Kunywa dawa za kikohozi na mafua kwa angalau siku tatu ndipo utapona vizuri na kwa haraka zaidi. Usitegemee dawa moja kuwa nzuri kwako kwa ajili ya kila kikohozi au mafua yako, badili dawa kulingana na kikohozi na mafua uliyonayo.
No comments