Mvua kubwa inayoendelea Kenya yasababisha hasara kubwa
Watu waliokufa kutokana na mafuriko wakizikwa. Mafuriko hayo yalisababishwa na kupasuka kwa bwawa la Patel eneo la mji wa Solai karibu na Nakuru, Kenya, May 16, 2018.
Wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha nchini Kenya na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na maisha ya watu, Idara ya Utabiri wa Hali Hewa imetoa ilani kwa wananchi kuhama baadhi ya maeneo hatarishi.
Idara hiyo imeendelea kusisitiza kuwa maeneo kadhaa kama vile eneo la bonde la Ufa, Magharibi, Kaskazini na maeneo ya kati nchini yataendelea kupokea mvua nyingi huku Shirika la Msalaba Mwekundu likionya kuwa huenda kukawa na matukio ya ugonjwa wa Kipindupindu na Malaria.
Maelfu ya watu wameachwa bila makazi huku shughuli za uchukuzi na masomo zikisitishwa.
Hata hivyo, serikali ya Kenya wiki hii imepokea msaada wa shilingi milioni hamsini kutoka serikali ya Uchina ukiwa ni msaada kwa watu walioathirika na mafuriko.
Mbali na tukio la kupasuka kwa bwawa la Patel huko Solai, Jimbo la Nakuru, wiki chache zilizopita ambako watu zaidi ya arobaini na saba walipoteza maisha na wengine wengi kuachwa bila makazi, maeneo mengi nchini Kenya yameendelea kupokea mvua yenye viwango vya juu zaidi ya wastani.
Rais Uhuru Kenyatta ametoa ahadi kuwa serikali yake itaendelea kuzisaidia familia zilizoathirika na mafuriko.
Mwanzoni mwa mwezi Mei takriban familia 500 ziliachwa bila makao katika ukanda wa Kano, maeneo ya Nyakach na Nyando magharibi ya Kenya baada ya mvua nyingi kunyesha katika eneo hilo na kusababisha Mto Nyando na Miriu kupasua kingo zake.
Katika jimbo la Kisii, shule ya msingi ya Itare ndiyo imekuwa hifadhi ya zaidi ya watu 70 ambao nyumba zao zilisombwa na mafuriko. Maeneo ya Njoro,Molo na Kuresoi katika jimbo la Nakuru, barabara zimeharibika huku shughuli za ukulima zikiathirika vibaya sana.
Barabara na baadhi ya mitaa imefurika maji mjini Nairobi japo athari hii inatokana na kile ambacho wasimamizi wa kaunti wanaeleza kuwa ni kuwepo kwa ujenzi mbovu wa miundombinu isiyoweza kukidhi majitaka. Mvua ikinyesha kwa wingi, barabara za katikati ya jiji la Kenya hujaa maji huku watu wengine wakilazimika kutumia mikokoteni kuvusha wasafiri.
Tangu Jumapili, kutokana na mvua nyingi inayoendelea kunyesha katika jimbo la Turkana, viwango vya maji katika daraja la Kainuk vimeripotiwa kupanda hali ambayo mpaka sasa inawaogopesha wakazi wa eneo hilo huku barabara ya Lodwar-Kakuma karibu na daraja la mto Kalawasse likiwa limeharibika.
Shirika la Msalaba Mwekundu ambalo limekuwa likitoa msaada wa chakula na malazi kwa wakazi walioachwa bila makao katika maeneo mengi nchini Kenya, linaripoti kuwa mvua ambayo ilianza kunyesha Kenya kuanzia Machi imeathiri zaidi ya familia elfu hamsini na vile vile kuonya kuhusu uwezekano wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu,chikungunya na Malaria.
Mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya Peter Ambenje kwa mahojiano ya kipekee na Idhaa hii anafafanua kisababishi cha mvua nyingi Kenya na maeneo mengine ya Afrika Mashariki.
Naye Peter Ambenje Mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya anasema takriban asilimia 70 ya ardhi ya jimbo hili ilifurika maji huku zaidi ya vijiji 32 vikisombwa na mafuriko na watu zaidi ya kumi wakiripotiwa kupoteza maisha yao.
No comments