MADHARA YA TATOO..!
Mara nyingi alama hizi zinaweza kuwa ni michoro ya maua, picha za watu au wanyama, ramani na hata wakati mwingine inaweza ikawa haieleweki.
By Clifford Majani, Mwananchi
Siku hizi hapa nchini ni jambo la kawaida kuona watu hasa vijana wakiwa wamejiremba miili yao kwa michoro, maarufu kama tattoo.
Michoro hii huwa inalenga sababu na maana mbalimbali, ingawa jambo hili kwa vijana huonekana kama kwenda na wakati. Wakati mwingine michoro hiyo huandamana na imani za kishirikina katika kutekeleza malengo fulani.
Mara nyingi alama hizi zinaweza kuwa ni michoro ya maua, picha za watu au wanyama, ramani na hata wakati mwingine inaweza ikawa haieleweki.
Alama au michoro zisizoeleweka huchorwa maeneo ya wazi au yaliyojificha ambayo huonekana pale tu mtu akiwa amevua nguo.
Alama kwenye maeneo ambayo huweza kufichwa ni kama vile misuli ya mikono, mabega, kifua, tumbo, mgongo, mapaja, makalio na maeneo yanayozunguka sehemu za siri. Maeneo ya wazi ni paji la uso, mikono, vidole, visigino au miguuni.
Michoro hii huweza kuchorwa kwa ajili ya kipindi fulani tu au ya kudumu kulingana na malengo na kusudio la mhusika.
Yale ya muda huweza kuchorwa kwa ajili ya tukio kama vile michezo, kuolewa ama sherehe mbalimbali ambazo huhusisha wanawake.
Kuna wanaotumia rangi zinazotokana na mimea ya kawaida na wengine hutumia dawa maalumu zinazouzwa madukani pamoja na vifaa vya kuchorea.
Wanasayansi wa afya ya jamii wanaonya kuwa michoro iliyotokana na rangi za madukani pamoja na vichoreo vyake, inaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa wahusika.
Baadhi ya rangi zinazotumika kuchora mapambo mwilini zinaweza kusababisha mzio wa ngozi katika eneo la mwili mahali palipo na tattoo. Mzio huu unaweza kutokea kipindi kirefu baada ya kuchora tattoo.
Tafiti nyingi za kitabibu pia zinaonesha kwamba, wino au rangi za tattoo zinaweza kusababisha uambukizo wa bakteria aina ya mycobacterium cholonae .
Bakteria hawa wanaweza kusababisha magonjwa ya ngozi na nyama za mwili, matatizo ya njia ya mkojo, tatizo kwenye mfumo wa kupumua, magonjwa ya uambukizo kwenye mifupa, uambukizo katika nyama za moyo, homa ya uti wa mgongo na tatizo la macho.
Vilevile vifaa vinavyotumiwa kuchora mapambo hayo hutumika kwa watu mbalimbali kwa wakati mmoja bila utaalamu sahihi wa kuvisafisha na hivyo kuweka uwezekano wa vimelea vya ugonjwa fulani kubebwa na kuhamishiwa kwa wengine.
Hali hii inaweza kusababisha uambukizo wa magonjwa yatokanayo na virusi hatari kama vile virusi vya Ukimwi, virusi ninavyosababisha homa ya ini (hepatitis B na C) au virusi vya malengelenge (herpes simplex virus ). Kumbuka wakati wa kuchora tattoo, ngozi hutobolewa kwa mashine au sindano hadi kuifikia sehemu ya ndani kabisa.
Vifaa hivyo pia vinaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa kama vile pepopunda ( tetanus ), majipu na hata kaswende.
Kwa sababu hiyo, katika baadhi ya nchi zilizoendelea mtu anapochora mwili wake tattoo, haruhusiwi kumwongezea mtu mwingine damu yake hadi mwaka mmoja upite baada ya kuweka michoro hii.
Hii ni kutokana na hofu ya uambukizo wa maradhi anayoweza kupata wakati wa kuweka tattoo yasijekuambukiza mtu mwingine.
Lakini pia mapambo haya yanaweza kusababisha manundu ya ngozi (keloids ), kupata hisia ya kuungua mwili wakati wa uchunguzi wa kitabibu kwa kutumia mionzi (Magnetic Resonance Imaging, MRI) na saratani mbalimbali. Miongoni mwa saratani hizo ni pamoja na saratani za limfu na tishu (primary non-Hodgkin lymphoma na leiomyosarcoma ).
Katika utafiti uliofanywa mwaka 2006 na Paradisi A, akishirikiana na timu ya watafiti wengine, ilithibitika kuwa tattoo pia zinaweza kusababisha saratani za ngozi. Dk Elizabeth Tanzi, daktari bingwa na mtafiti wa magonjwa ya ngozi, anasema kuwa matatizo ya kiafya yatokanayo na kuchora tattoo, siyo jambo geni.
Dk Tanzi anaongeza kusema kuwa licha ya kusababisha uambukizo na mzio kwenye ngozi, wino wa tattoo pia unaweza kusababisha uvimbe wa ngozi wakati wa kufanya kazi kwenye jua kali.
Tafiti mbalimbali za kisayansi zimeonyesha kuwa aina nyingi za wino unaotumika kuchorea tattoo, una madini ya sumu kama vile zebaki, nickel, lithium, cadmium sulfite, lead na benzo (a) pyrene .
Sumu hizi zinajulikana kwa uwezo wake wa kusababisha saratani na kudhuru tishu za mfumo wa limfu (lymph nodes ) katika mwili wa binadamu.
Mnamo mwaka 2005, Fredrik Ljungderg, mchezaji wa mpira wa miguu wa timu ya Arsenal wakati huo, alipata madhara makubwa katika mfumo wa limfu kutokana na tattoo kiasi cha kupata mitoki na kufanyiwa upasuaji.
Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyoandikwa na Sam Coates mwezi Mei, 2005 katika mtandao wa
www.timesonline.co.uk.
Matatizo ya kisaikolojia pia yanaweza kutokea pale sababu au mtindo wa kuchora mapambo kwenye ngozi unapopitwa na wakati na akatamani kuondoa alama hiyo bila mafanikio.
Akili ya vijana wengi inaendelea kukua na kupitia katika mabadiliko ya maamuzi kila mara na kutaka kwenda na wakati.
Mitindo ya mapambo mengi ya urembo hubadilika kulingana na mabadiliko ya kitamaduni katika jamii yoyote ile.
Hina nyingi za madukani zinazotumika kuchora tattoo au mapambo ya ngozi ya muda mfupi na dawa za kubadili rangi ya nywele, pia zina sumu ya para-phenylediamine (PPD) ambayo inaweza kusababisha mzio wa ngozi au mzio katika njia ya hewa.
Mzio utokanao na hina hii unaweza kumfanya mtumiaji aathirike pale anapotumia dawa za hospitalini zenye kemikali aina ya sulfa na baadhi ya dawa za nusu kaputi zitumikazo wakati wa upasuaji hospitalini.
Lakini pia baadhi ya kemikali katika wino wa tattoo zinapotumiwa wakati wa ujauzito, zinaweza kumsababishia mtoto ulemavu wa kuzaliwa nao.
Wagonjwa wa kisukari na wale wenye upungufu wa kinga mwilini wanaojitambua, wajiepushe kuchora tattoo kwa sababu zinaweza kuwasababishia vidonda visivyopona kwa haraka.
No comments