Breaking News

USIKURUPUKE FANYA HIVI KUJUA BIASHARA INAYOLIPA ENEO ULIPO


Leo tutashauriana changamoto ya jinsi ya kujua biashara inayolipa kwenye eneo unaloishi. Moja ya changamoto kubwa ambayo watu wengi wanakutana nayo ni kushindwa kujua biashara gani wafanye kwenye maeneo yao ili kuweza kupata faida.

 Mara nyingi watu wamekuwa wakiomba ushauri sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye mitandao kuhusu biashara gani wafanye kwenye maeneo yao.

Leo nitakushauri biashara unayoweza kufanya kwenye eneo lolote unaloishi na kupata faida kubwa sana.

Je ni biashara gani inayolipa?
Kwa maoni yangu biashara yoyote inalipa kama itafanywa kwa eneo sahihi, wakati sahihi kwa kutumia mbinu sahihi na kuwa na uvumilivu wa kutosha. Katika makala hii ndio biashara inayolipa sana nilizungumzia ni jinsi gani unaweza kuanzisha biashara popote na ukatengeneza faida kubwa.

Tatizo kubwa la watu kushindwa kupata faida kutokana na biashara wanayofanya na kuishia kuacha linaweza kutokana na mambo yafuatayo.

1. Uchaguzi mbaya wa biashara.
Kama unafanya biashara ambayo hakuna wanunuzi na huwezi kutengeneza wanunuzi kwenye eneo unalofanyia biashara ni dhahiri kwamba utashindwa.

2. Kuiga.
Kukopi na kupesti imekuwa ndio mtindo wa biashara nyingi zinazoanzishwa. Watu wengi wanaanzisha biashara sio kwa sababu wamefanya utafiti na kujua soko linataka nini na wao wanaweza kutoa nini, bali kwa kuangalia wafanyabiashara wengine wanafanya nini na wao kuiga. Hii ni njia rahisi sana ya kushindwa kwenye biashara hasa kama mtaji wako sio mkubwa sana.

3. Kutokujifunza.
Watu wengi sana wanafanya biashara kwa mazoea. Tuko kwenye ulimwengu ambao unakwenda kwa kasi kubwa sana, ukizubaa kidogo unaachwa nyuma. Kama bado unafanya biashara zako kwa mazoea na hujifunzi mbinu mpya za kibiashara huwezi kufikia mafanikio makubwa.

4. Kukosa usimamizi wa kutosha kwenye biashara.
Kama huna muda wa kusimamia biashara yako ni bora uachane na biashara hiyo kwa sababu ni rahisi sana kupata hasara. Tabia ya binadamu ni kupenda kufanya kazi kidogo na kupata mapato makubwa, kama unafungua biashara na kuweka wasaidizi huku wewe ukiwa mbali au kuisimamia kidogo sana wasimamizi wako watakuingiza kwenye hasara.

5. Kukosa uvumilivu kwenye biashara.
Hakuna biashara yoyote ya thamani inayoweza kujiendesha na kuingiza faida kubwa chini ya miezi sita baada ya kuanzishwa. Biashara nyingi zinachukua mwaka mmoja mpaka miwili ndio ziweze kujitegemea na kuzalisha faida. Watu wengi wanafikiri kwa kuingia tu kwenye bishara unaanza kutengeneza faida, wanapokutana na changamoto wanaona suluhisho pekee ni kuachana na biashara hiyo.

Zipo sababu nyingi sana zinazopelekea watu wengi kushindwa kwenye biashara, hizo tano ni ambazo zinatokea kwa watu wengi na zenye adhari kubwa.
kitabu kava tangazo

Ufanye nini ili kuweza kutengeneza biashara yenye faida kutokana na eneo unaloishi?
Ili kuweza kutengeneza biashara yenye faida katika eneo unaloishi au unalopendelea kufanya biashara yako nakushauri ufanye mambo haya matano.

1. Fanya utafiti mdogo wa kujua biashara gani inayofaa kwa eneo hilo.
Ni muhimu sana kufanya utafiti mfupi ili kujua kama wazo lako la biashara linaweza kufanikiwa kwa eneo unalotaka kufanyia biashara. Sio kila wazo la biashara linaweza kutengeneza biashara kubwa na yenye faida. Kwa wazo lolote la biashara unalotaka kufanya jiulize na kujijibu maswali yafuatayo;
i/. Kuna soko la biashara yako, au kuna uwezekano wa kutengeneza soko.
ii/. Je soko lina ukubwa wa kutosha kukuwezesha kupata faida?
iii/.Je ni mbinu gani unaweza kutumia kuingia kwenye ushindani uliopo kwenye soko?
iv/. Ni rahisi kiasi gani kulifikia soko?
(Ninaposema soko namaanisha wateja, na sio soko kama eneo la kufanyia biashara)
Kwa kuweza kulijua na kulitathmini soko itakupatia mbinu za kuweza kuingia na kudumu sokoni.

2. Kuwa tofauti, kuwa mbunifu.
Kama kuna soko la biashara unayotaka kufanya ni dhahiri kwamba kuna watu wengine wanafanya biashara hiyo. Jiulize ni jinsi gani unaweza kujitofautisha na watu hao? Kama huna njia ya kujitofautisha nakushauri tu uachane na hiyo biashara maana utaumiza sana kichwa. Hakuna kitu kinachoumiza kichwa kwenye biashara kama ushindani usiokuwa na tofauti, kama kuna mwenye mtaji mkubwa kushinda wewe atakuondoa sokoni. Mara zote jua ni mbinu gani za kibunifu na za utofauti za kukuwezesha kukuza biashara yako.

3. Kua kwanza wewe ndio biashara yako ikue.
Inashangaza ni kiasi gani watu wanataka biashara zao zikue wakati wao wenyewe hawakui. Jua siri hii moja biashara yako haiwezi kukua kama wewe hukui. Ili wewe kukua unahitaji kujifunza kila siku kuhusiana na biashara unayofanya na biashara nyingine kwa ujumla. Tunaishi kwenye zama ambazo kujifunza kuko kwenye ncha za vidole, mtandao una kila kitu unachotaka kujifunza. Tembelea mitandao ya kujifunza kama  utapata mbinu bora ka kukuza biashara yako. Usitegemee kufanikiwa kwa kufanya biashara kwa mazoea, kujifunza ni muhimu sana.

4. Kuwa na usimamizi wa kutosha kwenye biashara yako.
Watu hawaaminiki kwenye fedha, ni tatizo sana kama umejinyima na kupata mtaji wa biashara halafu unaianzisha na kuwapa watu wengine waisimamie. Ni rahisi sana kushindwa au kupata hasara kwa njia hii. Ni vigumu sana kupata mtu anayeweza kuwa na uchungu na biashara yako. Nakushauri kama huna muda wa kufuatilia biashara yako kwa karibu ni heri utumie hiyo fedha yako kufanya mambo mengine yatakayokuingizia fedha kidogo kuliko kwenda kuipoteza huku ukiona.

5. Kuwa na uvumilivu.
Kama kila ukianzisha biashara na kuona hailipi unaacha na kuanzisha nyingine, utafanya kila aina ya biashara na hutaona mafanikio yoyote. Bishara sio rahisi kama watu wanavyoamini, biashara inahitaji uvumilivu na ustahimilivu. Ni vigumu na mara chache sana mtu anaweza kuanzisha biashara na akaenda vizuri bila ya kupata misukosuko. Kwenye biashara halisi kuna misukosuko mingi sana, unaweka mkakati mzuri na kujua faida itapatikana ila vinatokea vikwazo na kukurudisha nyuma. Katika nyakati hizi ndio unatakiwa kujifunza na kama ukivuka nyakati ngumu unakuwa umeongeza kinga kwenye biashara yako. Unapojifunza utajua ni wapi ulipokosea hivyo kuepuka kurudia makosa.

6. Usiitegemee biashara mwanzoni.
Kama nilivyosema hapo juu biashara inachukua mwaka mmoja na wakati mwingine miaka miwili kuweza kusimama na kujiendesha yenyewe na kutengeneza faida. Kipindi cha mwanzo cha biashara ni kigumu sana na hutakiwi kuondoa fedha yoyote kwenye biashara kwa matumizi yasiyo ya biashara. Usianzishe biashara na wakati huo huo ukaanza kuitegemea kwa kuishi, biashara hiyo itakufa.

Biashara ni nzuri sana kama umejipanga na unajua ni nini unafanya. Ila kama hujajipanga au umeiga, biashara inaweza kuwa ngumu sana kwako kiasi cha kuachana nayo kabisa. Kwa ushauri huu nafikiri unaweza kubadili mtazamo wako na mbinu za kufanya biashara.

No comments