Breaking News

MAMBO YAPAMBA MOTO MWENYEKITI KAMATI YA MAKINIKIA ATUMBULIWA NA BUNGE -VIDEO

Ripoti hiyo iliyosomwa jana na baadaye kukabidhiwa kwa Spika Job Ndugai na baadaye kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, pia imetaka wajumbe wa bodi ya mgodi wa Williamson Diamond Limited (WDL) waliohuhusika katika uingiaji wa mikataba ya uendeshaji mgodi huo wa almasi, wahojiwe na kuchukuliwa hatua stahiki.

Dodoma. Profesa Abdulkadir Mruma, ambaye alitikisa nchi kwa kutaja mawaziri na maofisa waandamizi serikalini waliohusika kusaini mikataba mibovu ya madini, ametajwa katika ripoti ya kamati maalum ya Bunge iliyoundwa kuchunguza biashara ya madini ya almasi.

Ripoti hiyo iliyosomwa jana na baadaye kukabidhiwa kwa Spika Job Ndugai na baadaye kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, pia imetaka wajumbe wa bodi ya mgodi wa Williamson Diamond Limited (WDL) waliohuhusika katika uingiaji wa mikataba ya uendeshaji mgodi huo wa almasi, wahojiwe na kuchukuliwa hatua stahiki.

Baada ya kufanya kazi kwa takriban miezi miwili, kamati hiyo, iliyoongozwa na mbunge wa Ilala, Mussa Hassan Zungu imebaini kasoro kadhaa katika udhibiti, usimamizi, umiliki na uchimbaji wa madini hayo ya vito katika mgodi huo pekee wa almasi nchini na ambao umekuwa ukizalisha madini hayo tangu mwaka 1940.

Akikabidhi ripoti hiyo katika hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Bunge jana mjini Dodoma, Zungu alisema watu waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za nchi, hawakuwajibika ipasavyo, baadhi wakiwa hawajui akaunti iliyokuwa inawekwa fedha ya mgawo wa Serikali.

Alisema wengine hawakujihangaisha hata kusoma ripoti za fedha wala mikataba, huku wengine wakishindwa kuheshimu taratibu na mikataba hiyo huku wengine wakikopa fedha bila ya kufuata taratibu.

Pia alisema kampuni ya Petrainayoendesha mgodi huo maarufu kwa jina la Mwadui, imekuwa ikikiuka mikataba, kufanya udanganyifu katika gharama za mitambo inayoingizwa nchini na pia kuwapo na uwezekano wa kampuni hiyo kutotaja kiwango halisi cha madini yanayouzwa nje na kubambika madeni, ambayo kamati imekataa kuyatambua.

Zungu alisema udhaifu katika mikataba ulisababisha hasara ya Sh95 bilioni na udhaifu wa usimamizi ulisababisha hasara ya Sh22 bilioni.

Alisema kutokana na udanganyifu huo, kamati imependekeza almasi isafishwe nchini badala ya kusafirishwa nje; Serikali iongeze kiwango cha hisa hadi kuwa sawa na mwekezaji ili mgawo wa mauzo ulingane na pia maofisa wa Serikali wahusishwe katika hatua zote.

Kuhusu waliopewa dhamana kutowajibika ipasavyo, Zungu alisema Profesa Mruma alilisababishia taifa hasara kwa kuruhusu madini yapotee kwa uzembe.

Alisema Mruma aliruhusu madeni ya kubambikiwa kwa kusaini nyaraka za kuyakubali na alipoulizwa alisema alisaini bila ya kuzisoma.

Alipoulizwa inakuwaje mtu msomi na aliyepewa dhamana na taifa kulinda rasilimali asaini nyaraka biola ya kuzisoma, alijibu kuwa anawaamini watu walioziandaa.

“Kamati imekataa kuyakubali madeni hayo kwa kuwa wahusika hawakufuata taratibu,” alisema Zungu.

Kiongozi mwingine aliyeonekana kutowajibika ni katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, James Mdoe, ambaye alihojiwa kuhusu fedha za mgawo wa Serikali zilizotakiwa kuingia kwenye akaunti iliyopo benki mkoani Shinyanga, lakini hakuwa na taarifa.

“Alituambia kuwa wala hana taarifa ya akaunti hiyo licha ya kuwepo katika wizara hiyo kwa takribani mwaka mmoja na nusu,” alisema Zungu.

“Hadi kamati inamaliza uchunguzi haikupata taarifa na utaratibu uliotumika wa namna ya kuhamisha fedha hizo.”

Zungu alisema taribani Sh100 bilioni zilikuwa zikitakiwa kuingia serikalini kupitia akaunti hiyo ya kanda.

Alisema pia kamati hiyo haijaridhishwa na udhibiti wa Serikali katika upotevu wa madini hayo katika hatua zote na kwamba wamegundua kuwa kuna uwakilishi katika mgodi huo wa Serikali lakini hawana nyenzo za kufanyia kazi.

Hata hivyo, alisema katika maeneo muhimu mawili ya uzalishaji wa madini ya almasi katika mgodi huo, hakuna uwakilishi wa Serikali.

Alisema kuna upungufu katika uthaminishaji wa madini ya almasi na kusababisha thamani isiyo sahihi kinyume na mwongozo.

“Manual (mwongozo) huu hautumiki. Mtu anatumia matakwa yake na mapenzi yake,” alisema.

Zungu alisema usafishaji wa mwisho wa madini hufanywa nje badala ya hapa nchini ili kuongeza thamani.

Alisema kamati iligundua kuwa mthaminishaji wa madini hayo hashiriki katika hatua zote mbili kulingana na mkataba wa wanahisa wa WDL.

Alisema usafishaji wa mwisho hufanyika nchini Ubeligiji, akisema mapato yatokanayo na almasi iliyosafishwa nje huwa madogo kulinganisha na nchi nyingine ambazo huuza bila ya kusafisha.

Alisema kuna zawadi ilitolewa zamani na mgodi huo miaka ya nyuma kwa kiongozi mmoja mkubwa, akisema thamani yake kwa sasa ni dola 200 milioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh400 bilioni za Kitanzania).

Pia alisema katika uchunguzi wao kwa siku mbili walizokaa mgodini hapo wameona makinikia ya almasi tani 1.5 ambayo yanaweza kutoa madini yenye thamani ya Sh2.3 trilioni.

Alisema hiyo inawafanya wahisi gharama za uchimbaji bado zimewekwa katika makinikia hayo kwa kuwa yalichimbwa miaka 50 na marehemu Wiliamson.

Petra inamiliki asilimia 75 wakati Serikali ya Tanzania asilimia 25 na utafiti uliopo hadi sasa unaonyesha kuwa mgodi wa Mwadui unaweza kuzalisha almasi hadi mwaka 2033, ingawa kuna uwezekano wa kuendelea kuzalisha miaka mingi ijayo.

Kwa mujibu wa ripoti ya fedha ya mwaka 2016, Petra ilipata dola 78.9 milioni za Kimarekani. Katika migodi yake yote duniani, Petra ilitoa mrabaha wa jumla ya dola 27 milioni za Kimarekani. Uzalishaji ulipanda kwa asilimia 5 mwaka 2016 hadi kufikia carrat 212.869 kutoka carrat 202, 265.

Mapato pia yaliongezeka kwa asilimia 27 hadi kufikia dola 78.9 milioni za Kimarekani kutoka dola 62.1 milioni Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ongezeko hilo lilitokana na kuuzwa kwa almasi aina mbili za kipekee za rangi ya waridi.

No comments