Breaking News

MARIA & CONSOLATA-RIPOTI MAALUMU: Pacha walioungana waeleza wanavyotamani watoto

 

 

Kwa ufupi

Jana tuliona jinsi pacha walioungana tumboni, Maria na Consolata wanavyoelezea matamanio yao ya ndoa na pia sakata la kufichwa hadi walipokuwa wakiandikishwa kuanza elimu ya msingi. Leo wanaendeleza mazungumzo yao kuhusu maisha ya ndoa na watoto.

Sasa endelea...     


Pengine usingependa kuendelea kusikiliza simulizi za Maria na Consolata, hasa inapofikia masuala yanayohusu faragha yao, yaani maisha ya ndoa.

Lakini kwa jinsi walivyo tayari kuzungumzia kila jambo ambalo pacha hao wanahisi watu wanaliona si la kawaida, ilikuwa rahisi kufahamu mengi kuhusu matamanio yao na mambo mengine ya faragha.

Maria na Consolata, pacha walioungana tumboni na ambao hivi sasa wamemaliza kidato cha sita wanasema kama kuna kitu maishani wanachopenda, hakuna kama kuwa na watoto.

Wanasema kwa kuwa wana ndoto za kuolewa, wanajua kuwa watafanikiwa kupata watoto.

“Ikiwa hatutaweza kupata ujauzito kutokana na hali yetu, basi tutalea watoto yatima na walio katika mazingira magumu,” anasema Consolata.

“Tunapenda sana watoto.”

Kama ilivyoelezwa awali, pacha hao wanachangia tumbo, lakini wana sehemu tofauti za siri huku wakichangia hisia katika moja ya miguu yao mitatu.

Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa daktari mfawidhi wa Hospitali Teule ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Kilawa Shindo, pacha hao wanaweza kuzaa ikiwa kizazi chao ni salama.

“Kuzaa ni usalama wa kizazi. Sasa kama mabinti hawa wana kizazi salama wanaweza kupata watoto,” anasema.

Asemavyo Mwalimu

Na mwalimu mkuu wa Shule ya Maria Consolata, Jefred Kipingi anaongezea kuwa wakifanikiwa kupata watoto, itakuwa ni muujiza mwingine wa kipekee ambao Mungu atataka kulionyesha Taifa.

“Tuendelee kuwatunza kwa hekima na upendo, tukiheshimu hisia zao ili tuendelee kuona miujiza ya Mungu. Binafsi nawaheshimu sana hawa watoto licha ya kuwa nilikuwa mkuu wao wa shule,” anasema Kipingi.

Dalili za wawili hao kuwa na uwezo wa kupata ujauzito zinaonekana; wanapata hedhi.

Wakati nilipopata nafasi ya kuzungumza nao mara walipohitimu darasa la saba mwaka 2010 nilitamani kujua itakuwaje watakapofikia muda wa kuanza kuvunja ungo.

“Huwa tunatumia siku tano kwenye hedhi. Tunaanza na kumaliza pamoja na huwa ni vigumu kujua nani anaenda na nani haendi hivyo huwa tunavaa taulo kwa pamoja,” anasema Consolata.

Anasema baada ya kuvunja ungo walikuwa wakisikia maumivu makali sana ya tumbo na kuna wakati walikuwa wakilazimika kuchomwa sindano za maumivu ili wapate ahueni.

“Ilikuwa hatuendi shule wiki nzima, lakini mwaka huu tuna maumivu ya tumbo ya kawaida sana. Hatuumwi kama zamani,” anasema.

Maria anasema maumbile yao ni kama wanawake wengine wa kawaida jambo, ambalo alisema linawafurahisha.

Kuungana kwa baadhi ya viungo vyao kumewafanya wapendane zaidi, tofauti na pacha wengine.

Kila mmoja anamuhisi mwenzake, na hilo limewafanya wafurahi na kuhuzunika pamoja.

Chumba wanacholala ni kisafi wakati wote, na wao wenyewe ndio wanaosafisha ikiwa ni pamoja na kutandika kitanda kwa ustadi. Chumbani kwao kuna redio na kwa kuwa hawapendi kupitwa na jambo lolote linaloendelea nchini na duniani kwa ujumla, huwa wanaiacha redio yao hewani usiku kucha.

Maisha yao

Kiujumla wanaishi maisha mazuri kwenye kituo chao cha Nyota ya Asubuhi na wanafurahia kulelewa kituoni hapo kwa kuwa licha ya kupewa mahitaji yote muhimu, wanapendwa.

Maria anasema hawana wasiwasi kutokana na malezi bora wanayopewa na kikubwa zaidi ni kufundishwa kumcha Mungu.

“Tuna kila sababu za kumshukuru Mungu na masista wanaotulea kwenye kituo hiki kwa kuwa wao ni sababu ya sisi kuishi na kufikia hatua hii kubwa kielimu,” anasema Consolata.

Kwenye nyumba yao waliyojengewa, yupo dada anayewalea. Anaitwa Fransisca Mlangwa, ambaye anasema hajawahi kujuta kuwa mlezi wao.

“Inapotokea wapo mbali nami huwa nawakumbuka. Nawaona kama wadogo zangu wa kuzaliwa. Hawa ni mabinti wa kipekee kwa kweli. Sijawahi kununa nikiwa nao, mara nyingi huwa wananichekesha na ninaona fahari kuwa mlezi wao,” anasema.

Francisca ni mwanafunzi anayesomea masuala ya mifugo katika kituo hicho.

Maria anasema nyumba hiyo imewekwa miundombinu yote muhimu inayowafanya wajisikie vizuri wakati wote wanapokuwa nyumbani.

“Tuna TV na simu ya mkononi ya kisasa hivyo tunasikia na kupata habari mbalimbali zinazoendelea nchini,” anasema Consolata.

Hufanya kila kazi

Maajabu mengine waliojaliwa pacha hawa ni namna viungo vyao vinavyofanya kazi kama mtu mwingine. Mkono mmoja wa Consolata huweza kushirikiana kufua na mkono mwingine wa Maria kwa mawasialiano kama ya mtu wa kawaida.

Wakiwa nyumbani hufanya usafi ikiwamo kuosha vyombo, kufua nguo, kufagia, kupiga deki na kazi nyingine zote muhimu.

“Tunapika kila aina ya chakula, tunakata mboga aina zote na kumenya nyanya,” anasema Maria.

Ukitafakari namna wanavyofanya kazi zao utagundua kuwa mapacha hao wana hisia moja.

Ushirikiano wao unashangaza. Hakuna anayemwambia mwenzake fanya kitu fulani, lakini mikono yao hujikuta ikifanya kazi kwa pamoja, kana kwamba si watu wawili tofauti.

Mfano, mkono wa Maria ukishika kisu, wa Consolata hushika kitu kinachotakiwa kukatwa bila ya wao wenyewe kuelekezana.

Na ikiwa watataka kufua nguo, wakishaandaa beseni, anayechukua sabuni hufanya hivyo bila kuelekezwa na mwenzake na baadaye mikono miwili hushirikiana kufua nguo moja.

“Sijawahi kumkata Consolata nikiwa nakata mboga hata kama yeye ndiye hushika. Hivi ndivyo Mungu alivyotuumba,” anasema Maria.     

No comments