Breaking News

Mrisho Gambo Kuwaburuza Kortini wadaiwa sugu kodi ya Majengo, Arusha

WADAIWA sugu wa kodi ya majengo katika Jiji la Arusha wapo hatarani kuburuzwa mahakamani endapo wataendelea kukaidi kutolipa kodi hiyo katika kipindi cha mwisho wa mwaka wa fedha 2016/2017 unaomalizika Juni 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema hayo katika kikao chake na waandishi wa habari kuwakumbusha wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi hiyo mapema kabla ya hatua kazi hazijachukuliwa kwa ambao hawajalipa. 

Alisema wamiliki wote wa majengo wanatakiwa kulipa kodi hiyo kwa mujibu wa sheria, lakini hali hairidhishi kwani wengi wao hawajajitokeza kulipa wakati serikali inategemea fedha hizo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Aliongeza muda uliowekwa kwa ajili ya malipo hayo unaelekea ukingoni ambapo Juni 30 itakuwa ni mwisho. 

“Haiwezekani unamiliki nyumba halafu hutaki kuchangia kodi, ninatoa rai kwa wote kulipa kwa hiari kwa sababu baada ya hapo ni faini ambayo ni mara tano ya kiasi ambacho ungetakiwa kulipa kwa sasa au kupelekwa mahakani kwa mujibu wa sheria,” alisema. 

Naye Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Arusha, Apili Mbarouk, alisema mpaka mwishoni wa Mei walikuwa wamekusanya Sh. bilioni moja na kwa siku zilizobakia wanatarajia kukusanya zaidi. 

Aliongeza katika maeneo yote ambayo hayajapimwa na kufanyiwa uthamini wamiliki watalipa Sh. 15,000 kwa mwaka na kwa maeneo ambayo yamefanyiwa uthamini wamiliki watalipa kadiri ya thamani ya majengo yao. 

Alisema wataanza ukaguzi katika maeneo yote ya mji huo, mfanyabiashara atakayebainika hatoi risiti atapigwa faini ya Sh. milioni 3 mwananchi ambaye atanunua bidhaa bila kudai stakabadhi atatozwa faini ya Sh. 30,000.30.

No comments