Breaking News

Rais Magufuli Atoa Msimamo Mkali

Rais John Magufuli ametoa msimamo mkali dhidi ya watu wanaobeza jitihada za kuleta maendeleo zinazofanywa na Serikali.

Amesema Serikali ipo na haijalala, akisisitiza kwamba simba aliyelala asisogelewe na kuchezewa mkia.

Pamoja na hayo, Rais amewataka Watanzania kutembelea kifua mbele kwa kuwa nchi iko vizuri na ina uwezo mkubwa kiuchumi.

Alisema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mfumo wa rada za kuongoza ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

“Uwezo wetu ni mkubwa mno na wa ajabu, tumeweza kufanya mambo makubwa ndani ya muda mfupi, watu wanashangaa Tanzania tumewezaje kununua ndege bila kukopa,” alisema.

Rais alisema, “Ni sababu hiyo inawafanya watu wenye wivu waumie mno, niliposema nitanunua ndege wakasema nitapata wapi fedha, nikawaambia fedha zangu zipo kwa mafisadi na nilisema watazitoa kwa kutaka au kutotaka hata kwa nguvu nitawabana watazitapika.”

Alisema haumizwi na maneno ya watu kwa kuwa lengo lake ni kuiletea maendeleo Tanzania.

“Wapo watu duniani hata umfanyie vipi haridhiki, niwaambie wazi Watanzania wenzangu tupo pazuri mno, kwa Afrika ni miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi. “Ninafahamu hata makanisani zaka zimepungua kwa kuwa nyingine zilikuwa zinatolewa na mafisadi,” alisema.

Rais Magufuli pia alivipongeza vyombo vya ulinzi kwa kuendelea kuimarisha ulinzi nchini.

Alisema, “Vyombo vya ulinzi vinafanya kazi kubwa sana hata Kibiti unakwenda bila wasiwasi, awali mauaji yalikuwa yakitokea na hatukuona mtu analaani wala kutoa waraka wowote, lakini sijali kwa kuwa nimekabidhiwa Serikali na Watanzania.

“Sitaki kusema sana kwani hakuna lolote lakini niseme Serikali ipo na wala haijalala. Usione simba amelala ukasogea kuchezea mkia wake,” alisema.

Mradi wa mfumo wa rada

Mfumo huo wa rada za kuongozea ndege uliozinduliwa na Rais Magufuli, unajengwa katika vituo vinne vya JNIA, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe na unafanywa na Kampuni ya M/S Thales Las France SAS ya Ufaransa ukigharimu Sh67.3 bilioni ambazo zote zinazotolewa na Serikali ya Tanzania.

Akizungumzia ujenzi wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari alisema unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 hiyo ikimaanisha kwamba mradi huo ulioanza kujengwa Novemba mwaka jana utakamilika Mei mwakani.

Alisema asilimia 20 ya Sh67.3 bilioni tayari zimelipwa kwa mkandarasi.

Johari alisema anga ni ghali, hivyo linahitaji fedha nyingi na kwamba kukamilika kwa mfumo wa rada Tanzania itakuwa na uwezo mkubwa wa kudhibiti anga, kuongeza ufanisi zaidi na utavutia wageni kuja nchini kutalii.

“Tumesitisha kampeni za nchi jirani kutaka kukasimiwa (kusimamia anga) kutokana na wao kuwa na mifumo mizuri na kuanza kwa mradi huu tumezuia harakati hiyo,” alisema Johari.

Alisema mradi huo unagharimiwa na Serikali Kuu kwa asilimia 55 na asilimia 45 ni fedha kutoka TCAA.

Kuhusu mradi huo, Rais Magufuli aliitaka wizara na TCAA kuhakikisha mkandarasi anasimamiwa ipasavyo ili ujenzi huo ukamilike hata ikiwezekana kabla ya wakati.

“Niviagize vyombo vyote vya ulinzi kuimarisha ulinzi katika viwanja na kuzunguka viwanja vyote,” alisema.

Rais Magufuli alisema kwa sasa kuna rada moja tu. “Uwezo wake ni kuhudumia asilimia 25 ya anga yetu na kwa sasa imechakaa na huo ndiyo ukweli wenyewe.”

Alisema kukamilika kwa ujenzi huo kutarahisisha ulinzi na kuongeza mapato kwa kuwa, “Tozo ya Sh2.2 bilioni ni gharama za kuongoza ndege kwa nchi tulizokasimiwa.

“Haiwezekani unakuwa na ndege zinaongozwa na nchi kutoka nje, ndege inaongozwa kutoka Dar es Salaam kwenda Tabora na nchi ya nje, hatuwezi kuwa na Taifa la aina hii, tunataka tuwe na rada yetu,” alisema.

Aliwapongeza watumishi wa TCAA kwa jitihada wanazozifanya na hasa kuongeza mapato yao na kuvuka lengo.

Pia, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa aliipongeza TCAA kwa jitihada za kugharamia mradi kama huo na kuagiza mashirika mengine kuige mfano wa mamlaka hiyo.

Alisema wanataka kuifanya JNIA kuwa njia panda ya usafiri wa anga na viwanja mbalimbali vitakarabatiwa kwa fedha za ndani.

Kuhusu ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Rais Magufuli alisema mkandarasi anasuasua na kwamba fedha si tatizo.

Alimwagiza, Profesa Mbarawa kwenda kusimamia ili mkandarasi huyo afanye kazi usiku na mchana.

Waraka wawaibua Ma-RC

Katika hafla hiyo, wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro waligusia waraka wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na ule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) uliotolewa Machi 24.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema, “Tumesikia katika mikoa mingine kuna waraka, hapa kwetu hakuna waraka, watu wamesali bila matatizo.”

Alisema kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa wakitoa kauli za kichochezi, “Wanatoka katika mikoa yao kuja kwetu, ifike mahali tuangalie sheria zetu ili wawe wanatoa matamko hayo wakiwa hukohuko kwao.

Alisema, “Mkoa wetu uko shwari, hauna chokochoko.”

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema, “Mwanza iko tayari, hakuna tangazo lolote limetoka, tutaendelea kuwa salama.”

Alisema wataendelea kufanya kazi kwa kutekeleza miradi ikiwamo barabara zinazounganisha nchi jirani.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alisema rada hizo zitaongeza usimamizi wa anga hasa kwa kuwa ni miongoni mwa mikoa ya mipakani.

Kuhusu matamko ya waraka, Anna alisema, “Naona mkuu wa mkoa wa Mwanza na Dar es Salaam wamenichokoza na matamko, yote yameanzia Kilimanjaro na yataishia hapo... tutapima kila hoja na kukuletea taarifa.”

No comments