WALIOONDOLEWA KWA VYETI VYA DARASA LA SABA WATAKA MAFAO YAO
Moshi. Wafanyakazi 66 walioondolewa kazini katika Hospitali ya Rufaa KCMC mjini hapa, kutokana na kuwa na vyeti vya darasa la saba wamemtaka mwajiri kuwalipa mafao yao. Miongoni mwa waliositishiwa ajira ni aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Mhumba.
Pia, wamemtaka mwajiri kuwalipa mishahara ya miezi saba tangu waachishwe kazi mwezi Juni, wakidai utaratibu wa kuwaondoa haukufuatwa, hivyo wao bado ni wafanyakazi halali.
Mhumba alidai hawakuajiriwa na Serikali, bali KCMC ambayo alisema ina uwezo wa kuwalipa fedha kutokana na mapato yake.
Alidai KCMC inakwepa jukumu la kuwalipa na badala yake inasema inasubiri mwongozo kutoka serikalini.
Mhumba alisema hayo jana mbele ya msuluhushi na mwamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Mkoa wa Kilimanjaro, Godwin Migire.
Aliyekuwa mlinzi wa hospitali hiyo, Petro Shaluo alisema kwa miaka zaidi ya 10 aliyoitumikia hospitali hiyo alilinda mali kwa uaminifu, lakini leo anashangaa kuonekana hafai.
No comments