Breaking News

TANESCO YATOA UFAFANUZI TATIZO LA LUKU

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limewatoa hofu wateja wake juu ya mfumo wa ununuzi wa umeme kwa njia ya luku na kusema kuwa kwa sasa upo sawa na wanaweza kununua katika mifumo iliyozoeleka.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Kaimu Meneja wa Teknolojia na Mawasiliano(TEHAMA) wa Tanesco, Demetruce Dashin amesema kuwa kulitokea tatizo dogo la mfumo wa ununuzi wa umeme kwa njia ya Luku kutokana na wataalamu wa shirika hilo walipokuwa wakiamisha mitambo hiyo kutoka ofisi ya Zamani kwenda sehemu nyingine.

Bw. Dashina amefafanua kwamba kufuatia taharuki ya tatizo la kimtandao lililotokea jana kupelekea watu kupata shida katika ununuzi wa umeme Shirika la Umeme nchini (TANESCO) limesema tatizo la kimtandao ambalo lilianza jana kufuatia hitilafu katika mfumo limeshughulikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo wanatarajia kumaliza tatizo hilo ndani ya siku chache.

“Jana tulikuwa tunafanya uhamisho wa mfumo wa luku kwende katika ofisi zetu mpya hivyo ikawalazimu wateja wetu kupata usumbufu kidogo, lakini kuanzia saa saba mfumo huo umekaa sawa na wateja wanaweza kununua umeme kama walivyokuwa wanafanya hapo awali bila shida yoyote mara baada ya marekebisho ya kiufundi” amesema Dashina

Aidha Bwana Dashina amesema mpaka sasa wataalamu wanaendelea na zoezi  la ukarabati ambalo limekamilika kwa asilimia kubwa ambapo wanaendelea na uhamishaji mitambo kutoka ofisi zao za zamani na kuweka kwenye ofisi mpya.

Kwa upande wake Kaimu Meneja  Uhusiano wa Tanesco Leila Muhaji amewaomba radhi wananchi kwa usumbufu uliojitokeza na kuwasisitiza kuwa sasa wanaweza kununua katika mifumo iliyozoeleka.

Muhaji amesema kuwa Tanesco inatambua umuhimu wa umeme hivyo kuwataka watanzania kuwa na imani na shirika lao kwani lipo kwa ajili ya kuwahudumia  kama inavyohitajika na kuongeza kwamba tukio hilo la jana limesimamisha shughuli nyingi ambazo zimerudisha nyuma shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kuwahakikishia wananchi tatizo hilo kumalizika haraka iwezekanavyo.

No comments