Breaking News

SHULE YA CCM YAZUA MTAFARUKU BUNGENI


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo amesema shule ya wazazi ya Kamsamba iliyopo wilayani Momba inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM. 

Dodoma. Swali la mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde limezua kelele na kurushiana vijembe miongoni mwa wabunge bungeni.

Silinde alitaka kujua ni kwa nini Serikali isiirudishe kwa wananchi Shule ya Sekondari ya Kamsamba inayomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ili waitumie kwa ajili ya chuo cha ufundi au kidato cha tano.

Spika wa Bunge, Job Ndugai ndiye aliyesababisha kelele kutoka kwa wabunge wa kambi ya upinzani na wale wa CCM baada ya kuhoji ni kwa nini mbunge huyo anaomba shule ya sekondari ya CCM wakati vyama vya upinzani akikitaja Chadema hakina hata shule ya awali (chekechea).

Kauli ya Ndugai ilipokewa na wabunge wa upinzani kwa kupaza sauti kuipinga wakisema shule hizo zilijengwa wakati wa Serikali ya chama kimoja, hivyo ni mali ya wote. Wabunge wa CCM nao walipaza suti kuwapinga wenzao wa upinzani.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo amesema shule ya wazazi ya Kamsamba iliyopo wilayani Momba inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM.

Amesema shule hiyo ni ya kutwa ya wavulana na wasichana yenye kidato cha kwanza hadi cha nne na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 225 iwapo miundombinu yake itakamilika na kutumika.

Jafo amesema Serikali kupitia halmashauri itafanya mazungumzo na mmiliki wa shule hiyo ili kuona uwezekano wa kuyarejesha majengo hayo serikalini ili ianze kupokea wanafunzi.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo ameitaka Serikali na mbunge huyo kuona uwezekano wa kuikarabati Shule ya Mwalimu Julius Nyerere ili iwe bora badala ya shule za CCM.

No comments