Breaking News

Napambana na hali yangu: Haji Mwinyi

BEKI wa kushoto wa Yanga, Haji Mwinyi Mgwali, msimu uliopita ndiye aliyekuwa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kilipokuwa kikipambana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara. 

Alicheza mechi nyingi sana kumshinda mbadala wake Oscar Joshua waliyekuwa wakibadilishana naye katika nafasi hiyo. 

Hali hiyo ilitokana na uhodari aliokuwa akiuonyesha uwanjani kumshinda mpinzani wake ambaye pia huko nyuma ndiye aliyekuwa tegemeo ndani ya timu hiyo. 

Hata hivyo, baada ya  hivi karibuni Yanga kumsajili beki mwingine wa kushoto, Gadiel Michael, aliyetokea Azam FC na kuamua kuachana na Joshua, mambo yanaonekana kuwa magumu kwa Mwinyi. 

Tangu Gadiel ajiunge na Yanga, kwa sasa yeye ndiye anayeokana kuwa chaguo la kwanza la Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia George Lwandamina. 

Lwandamina amekuwa akivutiwa zaidi na uwezo mkubwa wa Gadiel ambao anauonyesha uwanjani kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi. 

Kutokana na hali hiyo, Mwinyi ambaye msimu uliopita alikuwa ndiye chaguo la kwanza la makocha hao kiasi cha kuonekana lulu kwa wapenzi na mashabiki wa Yanga kwa upande wa kushoto, tayari ameanza kuonekana kusotea namba na kumfanya aishie benchi kama ilivyokuwa kwa Joshua msimu uliopita. 

Hata hivyo, Mwinyi tayari ameshalibaini hilo na sasa yupo katika harakati kabambe za kuhakikisha anapambana na hali yake ili aweze kuinusuru nafasi yake hiyo ndani ya Yanga. 

Championi Jumatatu limezungumza na Mwinyi juu ya nafasi yake hiyo katika msimu huu kuwa finyu pamoja na hali ya ushindani wa namba aliyonayo dhidi ya Gadiel. 

Anamzunguziaje  Gadiel 

“Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kila jambo kwani yeye ndiye mweza wa yote hapa duniani. 

“Lakini pia napenda kuupongeza uongozi wangu wa Yanga kwa usajili mzuri ilioufanya msimu huu na zaidi kwa kumsajili Gadiel ili aje kunipatia changamoto kama hii. 

“Kusema kweli usajili huu wa Gadiel tayari nimeanza kuiona faida yake lakini pia kwa timu yangu. 
“Hakika nitatakiwa kupambana zaidi ili niweze kuendana na kasi ya mpinzani wangu lakini pia uhakika wa nafasi katika kikosi cha kwanza. 

“Gadiel yupo vizuri na ninaikubali kazi yake kwani nimepata changamoto nzuri kwa ajili ya maendeleo ya soka langu la baadaye. 

“Ili niweze kurudisha nafasi yangu hiyo natakiwa kuongeza bidii yangu mazoezini ili niongeze kiwango changu. 

“Natakiwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu ili niweze kutimiza ndoto zangu hizo, lakini pia natakiwa kuzingatia mambo yote ambayo mchezaji anatakiwa kuyafuata kwa ajili ya kulinda kiwango chake. 

 “Pia napaswa kujitambua kuwa mimi ni nani na ninatakiwa kufanya nini katika soka ili niweze kufikia malengo yangu na mengine mengi niliyojiwekea kwa faida ya klabu yangu hii lakini pia kwa taifa langu pamoja na maisha yangu ya binafsi. 

“Pia natakiwa kuwa mwepesi wa kuyapokea yale yote nitakayokuwa nikipewa na kocha wangu, hasa yale yanayohusiana na mambo ya kiufundi, nikifanya hivyo ninaamini nitakuwa vizuri kabisa na kuweza kukabiliana na hali ya ushindani iliyopo hivi sasa ndani ya klabu yangu, lakini pia itanisaidia katika ndoto zangu za kucheza soka la kimataifa,” anasema Mwinyi. 

Kuhusu ubunifu 

“Ninajitahidi kuongeza ubunifu pindi ninapokuwa uwanjani ili uweze kunisaidia kuongeza kiwango changu. 

“Nimejifunza mambo mengi kutoka kwa baadhi ya wachezaji ambao wanafanya vizuri zaidi  kimataifa kwani wengi wao hawategemei tu mafunzo ya makocha wao ila nao hujitahidi kuwa wabunifu. 

“Kwa hiyo na mimi najitahidi kuwa mbunifu wa mbinu mbalimbali ambazo nikizichanganya na mafunzo ya makocha wangu, zitanisaidia kutimiza ndoto zangu,” anasema Mwinyi ambaye alisajiliwa na Yanga akitokea KMKM ya Zanzibar. 

Kuhusu mambo ya nje ya uwanja 

“Kuhusiana na mambo mengine ya nje ya uwanja, mimi ni mtu wa kawaida kabisa ninayeishi kwa kuzingatia maadili na tamaduni za Mtanzania lakini pia maagizo ya Mungu. 

“Situmii kilevi chochote lakini pia siyo mtu wa starehe, zaidi ninapokuwa nyumbani muda wangu mwingi nautumia kwa kujifunza mambo mbalimbali ya soka kwa kuangalia video za wenzangu wanaonizidi uwezo. 

“Kama kuna tuhuma zozote zile zinazosemwa dhidi yangu, hizo hazina ukweli wowote,” anasema Mwinyi ambaye ni mzaliwa wa Visiwa vya Zanzibar. 

No comments