Jiko la mama lishe lilivyoteketeza mamilioni ya fedha
Moto umeteketeza maduka sita ambayo licha ya mali iliyokuwemo, pia fedha taslimu Sh40.2 milioni zimeungua.
Jiko la mama lishe lililokuwa jirani na transfoma limesababisha moto uliounguza maduka sita yaliyokuwa kwenye nyumba moja eneo la Dongobesh wilayani Mbulu.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Chelestino Mofuga amesema maduka hayo yaliungua saa sita usiku wa kuamkia jana Jumapili.
Amesema moto huo umesababisha hasara ya mali yenye thamani ya Sh278.5 milioni na fedha taslimu Sh40.2 milioni zilizoungua.
Mofuga amesema chanzo cha moto huo ni jiko lililokuwa kwenye banda la mama lishe ambalo liko karibu na nyaya zinazoshikilia nguzo ya umeme ambako transfoma ipo.
"Nyaya za umeme zinazotoka kwenye nguzo zilishika moto ambao ulisambaa kwenye maduka sita yaliyo katika jengo moja kubwa," amesema.
Mkuu huyo wa wilaya na kamati ya ulinzi na usalama waliofika kutoa pole kwa wafanyabiashara hao, amesema maduka na mabanda yamejengwa jirani na nguzo za umeme.
"Nimeagiza wananchi wote wenye nyumba au mabanda ya biashara yaliyo jirani na nguzo za umeme kuyabomoa ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea," amesema Mofuga.
Pia, amemuagiza meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wa wilaya kukagua njia za kupitisha nishati hiyo na kuchukua hatua za kisheria kwa watu ambao nyumba zao zipo jirani na nguzo za umeme.
Mofuga amewataka wananchi kuacha kuweka fedha majumbani na badala yake watumie benki kwa kufungua akaunti kwenye taasisi hizo za fedha zenye matawi Mbulu mjini na Haydom.
Mkazi wa eneo hilo, Elias Tluway amemuomba mkuu wa wilaya kuzungumza na taasisi za fedha ili zianzishe matawi Dongobesh ambako mzunguko wa fedha ni mkubwa.
No comments