Breaking News

WALIOMPIGA RISASI TUNDU LISSU KUJULIKANA

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema watu waliopanga na kutekeleza shambulio la risasi dhidi ya mwanasiasa machachari wa upinzani, Tundu Lissu watajulikana muda si mrefu.

Ameliambia Mwananchi kwa njia ya simu akiwa Nairobi, Kenya, alipokwenda kusimamia matibabu ya Lissu kuwa shambulio hilo lilipangwa kwa muda mrefu na kwamba waliofanya hivyo hawawezi kujificha tena.

“Tukio hili lilipangwa na kuratibiwa kwa muda mrefu. Kuna magari mengi yamekuwa yakimfuatilia Lissu kwa muda mrefu na hili jambo halikupangwa na mtu mmoja, limepangwa na watu wengi na baada ya muda kila kitu kitajulikana,” alisema.

Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) alishambuliwia kwa risasi zaidi ya 30 nyumbani kwake Area D mjini Dodoma muda mfupi baada ya kutoka kwenye ukumbi wa Bunge.

Watu wasiofahamika walilifuatilia gari lake tangu alipotoka bungeni saa saba mchana na alipofika nyumbani kwake alisita kushuka baada ya kuona gari hilo likiendelea kumfuata na ndipo aliposhambuliwa.

No comments