Mambo mazito aliyosema Kabudi
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi (pichani) amewasilisha kwenye Kamati Maalumu ya Bunge miswada miwili, huku akisisitiza wajumbe kujadili kwa manufaa ya taifa na si maslahi binafsi.
Miswada iliyowasilishwa jana ni Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi na ule wa Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017. Aidha, kamati leo zitaanza kukutana na wadau wa madini ili kukusanya maoni kabla ya muswada huo kujadiliwa na bunge katika vikao.
Alisema pia mabadiliko hayo yamelenga kupinga aina yoyote wa uharibifu na ubadhirifu, akisisitiza; “Hatuwezi kutumia maliasili hizi na utajiri huu kama sisi ndio wa mwisho kuishi katika nchi ya Tanzania na ndio maana waliotangulia hawakufanya hivi na ndio maana tunalileta hili. Na niwaambie tutalaaniwa kama tutajadili kwa maslahi yetu.
Akiwasilisha muswada wa pili wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi, Profesa Kabudi alisema mikataba hiyo haiendi kinyume na Katiba na ya misingi ya sheria za kimataifa kwa sababu Tanzania ni sehemu ya dunia. “Muswada huu unakusudia kutekeleza masharti ya Ibara ya 8, 9, 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 ambazo pamoja na mambo mengine zinampatia wajibu kila mtanzania kuhakikisha anashiriki kikamilifu kulinda mali na rasilimali za nchi kwa maslahi ya Watanzania kwa ujumla.
“Kwa kuzingatia wajibu huo kwa kila mtanzania na kwa kutambua wajibu wa Bunge kama chombo cha uwakilishi sheria inayopendekezwa imelipa nguvu bunge kupokea taarifa ya mikataba yote inayohusu maliasili ya nchi ambayo imeingiwa ili kujiridhisha kuwa masharti ya nchi yaliyomo kwenye mikataba hiyo yamezingatia maslahi ya watanzania na Taifa kwa ujumla na kuishauri serikali ipasavyo. Kabudi alisema kwa mujibu wa masharti yaliyopendekezwa baada ya kubaini kuna masharti hasi katika mikataba hiyo, Bunge linaweza kuitaka serikali kufanya majadiliano upya na upande wa pili wa mkataba ili kuondoa masharti hayo.
Alisema pia muswada huo unaweka utaratibu wa namna ya kuanzisha majadiliano upande wa pili wa mkataba ili kuondoa masharti hasi kama yalivyobainishwa na Bunge kwa mujibu wa ibara ya 6(2) ya muswada, aidha sheria inayopendekezwa imeainisha masharti ambayo kwa taswira yake ni masharti hasi na hayapaswi kuwemo kwenye mikataba inayohusu rasilimali na maliasili za nchi.
Timu ya wataalamu ambayo iliundwa kufanya kazi hii na Rais ni Profesa Florens Luoga ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma) na amebobea katika Sheria za Kodi, Mikataba na Uwekezaji na Biashara za Kimataifa, Kasimiri Sumba ambaye ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Saidi Kalunde kutoka Kurugenzi ya Sheria katika Wizara ya Nishati na Madini na Honorius Njole, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi za Jamii (SSRA). Yaliyomo kwenye miswada hiyo Kuhusu Muswada unaopendekeza kutungwa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili, 2017, ni kuweka masharti yanayohusianisha misingi iliyomo katika mikataba na itifaki mbalimbali ambazo Jamhuri ya Muungano imetia saini na kuridhia.
Baadhi ya masharti yanayopendekezwa katika Muswada huu yanatokana na Azimio la Umoja wa Mataifa Namba 523(VI) la Januari 12, 1952 na Azimio Namba 626(VII) la Desemba 21, 1952, Azimio Namba 1314 (XIII) la Desemba 12, 1958, Azimio Namba 1515(XV la Desemba 15, 1960, Azimio Namba 1803(XVII) la Desemba 14, 1962, Azimio Namba 2158(XXI) la Desemba 6, 1966, Azimio Namba XXV la Desemba 11, 1970; na Azimio Na. 32 la Desemba 12, 1974.
Kwa kuzingatia masharti yaliyomo katika mikataba hiyo, Muswada huo unakusudia kuweka masharti yatakayohakikisha kwamba hatua yoyote inayochukuliwa kuhusu uwekezaji wa rasilimali za Taifa inatambua na kuzingatia haki ya Jamhuri ya Muungano kama Taifa huru na lenye mamlaka kusimamia na kutumia rasilimali zake kwa maslahi ya Taifa. Aidha, Muswada huo unakusudia kutekeleza masharti ya Ibara ya 27 ya Katiba ambayo pamoja na mambo mengine, inamtaka kila Mtanzania kulinda na kusimamia kikamilifu rasilimali za nchi kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Hatua zinazopendekezwa katika Muswada huu zinalenga kulinda mali na rasilimali za Taifa na kuondoa aina yoyote ya upotevu au ubadhirifu wa rasilimali za nchi. Kadhalika, katika muswada unaokusudia kupendekeza kutungwa kwa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ambazo ni Sheria ya Madini, Sura ya 23, Sheria ya Petroli, Sura ya 392, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura ya 148 na Sheria ya Bima, Suraya 394.
Marekebisho yanayopendekezwa yanalenga kuimarisha mifumo ya udhibiti na uwajibikaji katika sekta ya madini na petroli. Aidha, marekebisho katika Sheria za Kodi na Bima yanalenga kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato yanayohusiana na sekta ya madini na petroli. Aidha, Muswada mwingine wa mwisho unapendekeza kutungwa kwa Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba inayohusu Maliasili za Nchi.
Sheria inayopekezwa inakusudia kuweka utaratibu ambapo wananchi kupitia chombo chao cha uwakilishi yaani Bunge la Jamhuri ya Tanzania kupitia na kujadili makubaliano na mikataba yote inayohusu rasilimali za Nchi ambayo imefungana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kujiridhisha endapo masharti, makubaliano na mikataba hiyo haikinzani na maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Muswada huu unakusudia kutekeleza masharti ya Ibara za 8, 9 na 27 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambazo, pamoja na mambo mengine, zinampa wajibu kila Mtanzania kuhakikisha anashiriki kikamilifu kulinda mali na rasimali za nchi kwa masilahi ya Watanzania na Jamhuri ya Muungano kwa ujumla. Kwa kuzingatia wajibu wa kila Mtanzania na kwa kutambua wajibu wa Bunge kama chombo cha uwakilishi, Sheria inayopendekezwa imelipa nguvu Bunge kupitia mikataba yote inayohusu maliasili za nchi ambayo imeingiwa na Jamhuri ya Muungano ili kujiridhisha kwa masharti yaliyomo katika mikataba hayo yamezingatia maslahi ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.
No comments