Breaking News

Wanne wauawa Kibiti wakipambana na Polisi


WATU wanne wanaosadikiwa ni miongoni mwa wahalifu wanaofanya mauaji katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, wameuawa.

Wameuawa baada ya mapambano makali na Polisi, yaliyodumu kwa zaidi ya nusu saa katika kijiji cha Pagae, Kibiti. Kwa mujibu wa Mkuu wa Oparesheni Maalumu za Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi Liberatus Sabas, mapambano hayo yalitokea juzi saa tatu usiku barabara ya vumbi itokayo Pagae kuelekea Nyambunda. Kwamba askari Polisi wakiwa doria, walikutana na kikundi cha watu kinachokadiriwa kuwa na watu sita, ambao baada ya kuona gari la Polisi, walikimbilia vichakani na kuanza kuwarushia risasi Polisi. Alisema kutokana na hali hiyo, askari nao kwa ujasiri, walijibu kwa kurusha risasi.

Ndipo yalipoanza mapambano, yaliyodumu kwa zaidi ya nusu saa na Polisi kufanikiwa kuwazidi nguvu wahalifu hao. Katika tukio hilo, wahalifu wanne walijeruhiwa kwa risasi na walifikwa na mauti muda mfupi baadaye wakiwa wanapelekwa hospitali. Pamoja na kuwadhibiti wahalifu hao, polisi walifanikiwa pia kuokoa silaha mbili, magazini na risasi 17 zilizokuwa zinatumiwa na wahalifu hao.

“Katika tukio hilo tumefanikiwa kupata silaha mbili aina ya SMG na magazini mbili pamoja na risasi 17 zilizokuwa zinatumiwa na wahalifu hao na hii ni dalili kuwa tunaendelea vizuri na oparesheni yetu ambayo inashirikisha vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika wilaya hizi tatu za Mkuranga, Kibiti, na Rufiji,” alisema Sabas. Sabas alitoa mwito kwa wahalifu wengine, kuacha mara moja kufanya mauaji kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama, vinaendelea kufanya jitihada zote za kuhakikisha kuwa maeneo hayo, yanakuwa salama na wananchi wanaishi katika hali ya amani na usalama.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa, zitakazowezesha kupatikana wahalifu wengine ili kuhakikisha kuwa kila mmoja anaishi kwa usalama. Kwamba mtu ambaye atatoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa wahalifu hao, atazawadiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro fedha taslimu Sh milioni 10. Wakati huohuo, katika kuhakikisha vitendo vya mauaji katika ukanda wa Pwani vinamaliza, tayari Polisi Kanda Maalumu ya Pwani imeanza kufanya kazi huku Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Onesmo Lyanga akiteuliwa kuongoza kanda hiyo.

Lyanga ambaye awali alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani alitangazwa kuwa ndiyo atakuwa Kamanda wa Kanda hiyo na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), SimonSirro. Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Sirro alisema kwamba pamoja na kumteua Lyanga kuongoza kanda hiyo, lakini wananchi wanatakiwa kumpa ushirikiano kwani matatizo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji hayawezi kumalizwa na mtu mwingine bila ushirikiano wao.

Aidha, alisema kutokana na maeneo hayo kuwa mbali na mji na magari ya polisi hayawezi kufika, ameagiza kufanyika kwa doria za pikipili na kuwataka wazee wa maeneo hayo kuitisha mikutano ya vijiji na kuunda vikundi shirikishi. Alisema pia wamebaini wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijifanya wanakwenda kununua mashamba, lakini lengo lao ni kutaka kujua viongozi wa maeneo hayo, hivyo wananchi wanatakiwa kuwashirikisha viongozi kabla ya kupokea fedha ili ijulikane lengo la watu hao kama ni shamba au laa.

Awali, akizungumza baada ya kumaliza kuongoza kikao cha ndani cha viongozi wa polisi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema, vyombo vya usalama vinafanya kazi kubwa, hivyo wananchi hawapaswi kuwa na hofu. “Wananchi watambue vyombo vya usalama vinaendelea vizuri sana na kazi yake ya kuhakikisha tatizo la mauaji ya Kibiti na kwingine linamalizika, hatuwezi kuweka wazi kila kitu lakini serikali inafanya kazi kubwa kuakikisha hilo linamalizika,” alisema Masauni.

Alisema kwa sasa serikali inafanya jitihada za kuboresha miundombinu ili kanda hiyo mpya iliyoanzishwa iweze kufanya kazi vizuri. “Bahati mbaya tu hamuandiki lakini hata jana, kwa kazi tunayofanya tumefanikiwa kuwadhibiti majambazi wawili kabla hawajatekeleza uhalifu wao…suala la kumaliza uhalifu Kibiti na Mkuranga ni suala ambalo halina mjadala ni suala la lazima,” alisema.

No comments