Waziri: Serikali yatoa siku saba walimu kupewa posho
SERIKALI imetoa siku saba kwa ajili ya halmashauri zote kuhakikisha walimu wa hesabu, sayansi na wataalamu wa maabara waliopangwa hivi karibuni wanapewa posho za kujikimu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angella Kairuki alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi (Chadema). Mkundi alitaka kujua ni lini serikali itawalipa stahiki zao walimu wa Hesabu, Sayansi na watalaamu wa maabara waliopangiwa vituo hivi karibuni. Alisema halmashauri zote zilizopokea walimu hao zinapaswa kuwapa posho za kujikimu ndani ya siku saba.
Akijibu swali la msingi la Mkundi aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kutoa posho za mazingira magumu kwa watumishi wa maeneo ya pembezoni, alisema, “Katika kutekeleza Sera ya Malipo ya Mishahara na Motisha iliyopitishwa mwaka 2010, mwaka 2012/13 halmashauri 33 za wilaya ikiwemo halmashauri ya Ukerewe ziliwezeshwa kuandaa miongozo ya kutoa motosha kwa watumishi.”
Alisema kutokana na mpango huo, halmashauri 29 ziliandaa na kuwasilisha katika ofisi ya wizara hiyo miongozo iliyobainisha aina ya motisha inayohitajika. “Utekelezaji wa miongozo hiyo kwa halmashauri zote 29 ulikadiriwa kugharimu Sh bilioni 331.087 kwa mwaka na utekelezaji wa miongozo hiyo, ulitarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha wa 2013/14 na haukuanza kutokana na ufinyu wa bajeti.
No comments