KESI YA VIONGOZI SIMBA YAAHIRISHWA TENA, AVEVA AIBUKA MAHAKAMANI, KABURU MGONJWA
MAKAMU wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameshindwa kutokea mahakamani leo kutokana na kusumbuliwa na maradhi na yupo katika zahanati ndogo ya gereza la Keko, Dar es Salaam kwa matibabu.
Kaburu na Rais wa klabu, Evans Aveva wanakabiliwa na mashitaka matano yakiwemo ya utakatishaji fedha, ambayo hayana dhamana na wote wapo rumande gereza la Keko tangu Juni 29.
Aveva aliletwa leo Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa tena mashitaka hayo kabla ya Hakimu Victoria Nongwa kuiahirisha tena kesi hiyo hadi Julai 31, mwaka huu.
Miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodaiwa kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni watuhumiwa hao kiasi cha dola za Kimarekani 300,000 (Zaidi ya shilingi milioni 700 za kitanzania).
Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwa Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
Shtaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka katika Benki ya Barclays Tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha fedha likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu anayedaiwa kumsadia Aveva kutakatisha fedha katika benki ya Barclays baada ya kughushi nyaraka.
No comments