Breaking News

Bosi wa trafiki ang'olewa

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni 

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amemvua madaraka Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani (RTO), Abdi Issango na kuamuru achukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na kushindwa kuwajibika katika nafasi yake. 

Pia Masauni amemwagiza Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Fortunatus Musilimu kuhakikisha anampangia kazi nyingine, ikiwa pamoja na kumhamisha mkoani hapa. 

Masauni, alifikia uamuzi huo jana, wakati wa ziara ya kushtukiza aliyoifanya stendi ya mabasi Mailimoja Kibaha mkoani hapa, kukagua utendaji kazi wa askari wa usalama barabarani. 

Alisema alipita katika stendi hiyo miezi mitano iliyopita na kutoa maelekezo kwa kamanda huyo, ikiwa pamoja na kuhakikisha anaongeza idadi ya askari wa ukaguzi wa magari, hasa mabasi yaendayo mikoani na kuwasimamia askari wa chini kuyakagua kwa uhakika, lakini hakufanya hivyo. 

“Miezi michache iliyopita nilikuja hapa, nikatoa maagizo kwa Kamanda Issango, nashangaa kuyakuta yaleyale, hakuna kilichofanyika, nimeamua kumvua nafasi yake kutokana na uzembe wa kushindwa kuwajibika,” alisema Masauni. 

Masauni alisema operesheni ya ukaguzi iliyofanyika Mkoa wa Pwani, inaendelea kufanyika nchi nzima. 

Aliwataka askari wa usalama barabarani kuhakikisha wanawajibika ipasavyo katika nafasi zao na atakayeshindwa Serikali haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria.

Masauni, alifanya ziara hiyo kwa kupitia Chalinze-Msolwa na Bagamoyo–Msata na kubaini kuwapo madereva bodaboda wengi ambao hawavai kofia ngumu (helmet) na kuagiza wale wote wasiovaa wakamatwe. 

Kwa upande wake, Kamanda Musilimu, alisema hayupo tayari kuona askari anafanya uzembe kazini kwa kushindwa kudhibiti makosa ya usalama barabarani na kuachwa.

No comments