Makamu wa Rais ayataka makampuni ya mafuta na gesi kununua bidhaa za ndani.
Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ameyataka makampuni yaliyowekeza katika sekta ya mafuta na gesi nchini kuhakikisha yanatekeleza sheria ya mafuta ya mwaka 2015 ya kununua huduma ama bidhaa ndani ya nchi ili kukuza uchumi wa taifa na kwamba serikali haipo tayari kuvumilia kikwazo chochote katika utekelezaji wa hilo.
Makamu wa Rais amesema hayo jijini Dare es Salaam wakati akizindua jumuiya ya watoa huduma za mafuta na gesi nchini ambapo amesema iwapo kuna ulazima wa kununuliwa nje ya nchi bidhaa ama huduma hizo makampuni ya nje yenye ubia na ya hapa nchini ndiyo yatumike.
Aidha Makamu wa Rais amewataka watoa hao huduma za mafuta na gesi kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa umoja hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na mahitaji makubwa ya huduma kutoka kwao ikiwemo zile zinatokana na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka mkoani Tanga mpaka Hoima nchini Uganda.
Naye Mwenyekiti wa jumuiya ya watoa huduma za mafuta na gesi balozi Ombeni Sefue amesema kupitia jumuiya hiyo wanategemea kuwa wataweza kufanya shughuli zinazohusiana na mafuta na gesi kisasa zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.
No comments