Kiongozi mwingine wa ACT-Wazalendo ang’oka
Kwa ufupi
Akizungumza na gazeti LA mwananchi kwa njia ya simu leo, (Jumamosi) Longopa, amesema haoni sababu ya kuendelea kuwa kiongozi wa chama hicho kwani kitampa wakati mgumu kuhamasisha wanachama wapya katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Mbeya. Katibu wa Chama ACT-Wazalendo Mkoa wa Mbeya, Bahati Longopa ametangaza kuachia wadhifa huo kwa kile alichodai kutoridhishwa na kitendo cha kuteuliwa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na kuitumikia Serikali ya Awamu ya Tano.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu leo, (Jumamosi) Longopa, amesema haoni sababu ya kuendelea kuwa kiongozi wa chama hicho kwani kitampa wakati mgumu kuhamasisha wanachama wapya katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
"Nimeamua kwa hiari yangu kuacha nafasi ndani ya chama kwani ukiona viongozi wa juu wanateuliwa kuingia katika Serikali iliyopo madarakani inayoongozwa na chama pinzani, sisi wa ngazi za chini tutapata wapi sauti ya kushawishi wanachama wapya kujiunga na ACT-Wazalendo,"amesema.
Kuhusu kujiunga na chama kingine cha siasa amesema kwa sasa ni mapema mno kuzungumzia hilo kwani ataendelea kukaa pembeni na kutojihususisha kwenye mambo ya siasa huku akitafakari nini cha kufanya.
Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Wilaya ya Mbeya, Ally Mbika alisema wamepata taarifa za chini chini, lakini kama chama bado hawajakabidhiwa barua yoyote kutoka kwa kada huyo kutamka kujiuzulu rasmi.
Amesema wanasubiri kukabidhiwa rasmi ili kuweza kulizungumzia kwa vyombo vya habari barua na viongozi wa chama watapitia katiba yao na kupata mwongozo na kuangalia namna ya kuziba nafasi hiyo mpaka Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Mbika amesema kuwa kujiengua kwa kada huyo ni pigo kwa chama kwani alikuwa ana mchango mkubwa wa ushawishi na kujenga umoja na mshikamano wa kweli wa ndani na nje ya mkoa.
No comments