Breaking News

Chadema wamchekelea Nyalandu, CCM wamponda


Kupitia akaunti zao za kijamii, wabunge wa upinzani wameonyesha kufurahishwa na uamuzi wa Nyalandu kujiondoa CCM na kuomba kujiunga Chadema.

 Wakati wabunge wa Chadema wakimpongeza aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu huku wakimtaka kujiandaa kwa harakati za siasa za upinzani, CCM wamebeza uamuzi wake wakieleza kuwa ni wa hasira na wa kujimaliza.

Kupitia akaunti zao za kijamii, wabunge wa upinzani wameonyesha kufurahishwa na uamuzi wa Nyalandu kujiondoa CCM na kuomba kujiunga Chadema.

Nyalandu alitangaza uamuzi huo juzi na kutoa sababu kadhaa za kufanya hivyo ikiwamo kile alichoeleza kuwa ni mwenendo usioridhisha wa sasa wa CCM.

Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule maarufu ‘Profesa Jay’ alisema, “Hongera sana my brother kwa ujasiri na kusimamia kile unachokiamini! Karibu sana kiumeni.

Mwingine ni Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya ambaye alisema, “Shikamoo Nyalandu.. raha sana.”

“Mhe. Nyalandu nikukaribishe kwenye siasa za upinzani Tz! Ni siasa tamu sana kwa wenye moyo mgumu! Ni ngumu sana kwa wenye moyo mwepesi,’’ ameandika Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Aliendelea “Mhe. Nyalandu karibu sana Chadema. Naamini utakuwa imara kukabiliana na siasa za chuki, ubaguzi na visasi zinazolikabili Taifa letu.’’

Vivyo hivyo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema, “Katika fani ya uandishi wa habari, taarifa ya Nyalandu ingeitwa scoop,” huku akihoji nani atakayefuatia.

Pia, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche alisema, “Hongera kaka kwa kukataa kuwa sehemu ya siasa za kishamba... siasa zilizojaa migawanyiko chuki visasi na vitisho.

“Umechukua uamuzi mgumu lakini sahihi, umeonyesha kwamba utu na ubinadamu ni muhimu kuliko fedha na vyeo, historia yetu itakukumbuka vizuri, karibu katika mapambano ya kudai haki na usawa.”

CCM wamponda

Wakati hao wakimsifia, CCM Mkoa wa Singida imesema sababu zilizotolewa na mbunge huyo hazina mashiko, isipokuwa kilichomsukuma kufukia uamuzi huo ni hasira za kukosa uwaziri.

Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Jamson Mhagama alisema, “Kwa maono yake ameona siasa za nchi haziendi vizuri na kuamua kwenda kusaka siasa zitakazompendeza, tunamtakia kila la kheri. Ila tunamwonya kuwa asitarajie tena kupata ubunge kupitia Chadema anakolilia kwenda, CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi mdogo ujao.

“Wananchi walimwamini katika vipindi vyote vinne kwa kumpa kura za kutosha za nafasi ya ubunge. Kupitia kura hizo, amesifika na kujulikana kila kona sasa ameamua kuwapa kisogo wakazi wa Jimbo la Singida Kaskazini, jina lake linaenda kufutika na hatasikika tena.”

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole naye alimponda akisema walishamweka pembeni kwa kuwa hakuwa mtu wa muhimu kwao.

Akizungumza juzi usiku katika kipindi cha Msemakweli kinachorushwa na Channel Ten, Polepole aliyekuwa akizungumzia mafanikio ya Rais John Magufuli kwa kipindi cha miaka miwili, alimtakia heri Nyalandu huku pia akisema amejimaliza mwenyewe.

“Ameondoka mwanachama mmoja wa CCM leo (juzi) amekwenda upinzani. Katiba yetu hii ya Jamhuri ya Muungano inasema kila mtu ana uhuru wa kujiunga na chama chochote. Tunaheshimu uamuzi wake, tunamkatia heri katika chama anakokwenda.

“Aliyeondoka leo ni ‘very insignificant’ yaani kwa Kiswahili hatujaona utofauti. Ndiyo maana sisi tumetoa maelekezo kwa Serikali kwamba, watu ambao hawakuweza kutukimbiza katika awamu ya nne kwenye maendeleo ya Taifa letu kwenye uongozi wa awamu ya tano wawekwe benchi kwanza. Sasa wamewekwa benchi,” alisema Polepole.

Katibu Mkuu wa ADA Tadea, John Shibuda alimpongeza Nyalandu kwa kutumia haki yake ya kikatiba na kufanya uamuzi kwa matakwa yake binafsi.

“Hivyo yanayozungumzwa sasa kutoka kwa wanasiasa mbalimbali ni kielelezo cha unafiki, tunaishi katika mfumo wa kusengenyana na wanaosema kuwa alikuwa siyo muadilifu wa kazi ndio wanamuona sasa kuwa sio muadilifu,” alisema Shibuda.

“Walivyokuwa naye walimkumbatia na kumsifia lakini sasa wanamuona ni mnafiki tena hafai.”

Imeandikwa na Gasper Andrew, Ibrahim Yamola, Elias Msuya na Hidaya Nyanga

No comments