Breaking News

JPM aagiza wahusika washughulikiwe

Rais John Magufuli akiwahutubia viongozi na wageni mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha  na Edwin Mjwahuzi Viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wakimsikiliza Rais John Magufuli alipokuwa akihutubia baada ya kupokea taarifa ya kamati ya pili ya uchunguzi wa madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Watu hao waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, wamebainika kuhusika katika kuikosesha Serikali mapato yatokanayo na madini kwa kuingia kwenye mikataba ambayo haina masilahi kwa Taifa.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza vyombo vya dola kuwachunguza na kuwachukulia hatua watu wote waliotajwa katika taarifa ya kamati ya pili aliyoiunda kuchunguza masuala ya kiuchumi na kisheria kuhusiana na mchanga wenye madini unaosafirishwa kwenda nje ya nchi yakiwamo makontena 277.

Watu hao waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, wamebainika kuhusika katika kuikosesha Serikali mapato yatokanayo na madini kwa kuingia kwenye mikataba ambayo haina masilahi kwa Taifa.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya kamati hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema mapendekezo yote 21 yaliyotolewa na kamati ameyakubali na kuagiza vyombo vya dola kuwachukulia hatua wote waliotajwa.

“Walio kwenye biashara zao kama Karamagi (Nazir) wafuatiliwe, wachunguzwe ili hatua zichukuliwe, nao watoe ushirikiano kwa vyombo vyetu jinsi walivyohusika. Kila waziri anayehusika akasimamie hili, kama ni Takukuru, kama ni TRA, kama ni Brela, mkalisimamie,” aliagiza Rais Magufuli.

Kiongozi huyo alionyeshwa kushangazwa na mauzo ya madini kutowekwa kwenye kumbukumbu zozote za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) licha ya thamani kubwa ya rasilimali hizo muhimu.

Alisema, “BoT sijui wanarekodi vipi kumbukumbu za madini, kwenye pamba wanarekodi, kwenye kahawa wanarekodi, huku kwenye madini kuna nini? BoT kuna PhD 17, but these are the results (lakini haya ndiyo matokeo).”

Rais Magufuli alieleza kushangazwa na baadhi ya wanasheria badala ya kuwa wazalendo na kulinda masilahi ya Taifa, wao wanatoa vitisho kwamba Serikali itashtakiwa kwenye mahakama za kimataifa kwa kuvunja mikataba.

Alisema yeye kama kiongozi yupo kulinda masilahi ya Taifa ndiyo maana amekuwa akichukua hatua pale unapotokea uzembe.

Pia alisema kuwa naye ni binadamu, ana moyo lakini hawezi kusimama kutetea maovu yanayofanywa na kampuni za madini.

Rais Magufuli alieleza kushangwa na watendaji wa wizara kushindwa kuchukua hatua yoyote kuhakikisha kwamba mitambo ya kuchenjua mchanga wenye madini inapatikana hapa nchini badala ya kuusafirisha nje ya nchi.

“Waziri pamoja na wataalamu wake hawana moyo wa kwenda huko nje angalau kuangalia smelter (mitambo ya kuchenjua) zinafananaje. Akili hiyo hawana. Wanaacha madini yetu yakisombwa tu. Hili soko ni la ajabu,” alisema kwa msisitizo.

Rais Magufuli aliwaambia wageni waliohudhuria hafla hiyo wakiwamo wakuu wa mikoa yote kwamba kamati iliambiwa kwamba tangu mwaka 1998 makontena ya mchanga 44,277 yalisafirishwa kwenda nje, lakini ikabainika kuwa yalikuwa ni makontena 61,320.

“Kiasi hicho cha madini nikikiweka kwenye malori ya tani saba saba, tunapata malori 177 hadi malori 304 kwa kadirio la juu. Thamani ya madini hayo ni Sh132.5 trilioni mpaka Sh229.9 trilioni,” alisema Rais Magufuli kwa hisia.

Aliwataka Watanzania kuwa kitu kimoja katika kupambana na vita hiyo ya kiuchumi na kwamba masilahi ya Taifa siyo siasa, bali ni ya watu. Alisema kama kiongozi ni lazima achukue uamuzi mgumu bila kujali unamgusa nani.

Wadau wazungumza

Wakizungumzia ripoti ya kamati na hatua iliyochukuliwa na Rais, wadau mbalimbali wamempongeza kwa kuonyesha dhamira njema kwa Taifa akitaka kuleta ukombozi wa kiuchumi kupitia rasilimali zinazopatikana hapa nchini.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk Jacob Chimeledya alisema ripoti ya kamati ni nzuri na inahitaji nguvu ya pamoja katika utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na kamati ya Profesa (Nehemiah) Osoro. “Mungu hajaumba Tanzania iliyo maskini, ina rasilimali nyingi. Lakini katika kusimamia hizi rasilimali unahitajika umakini wa hali ya juu ili tusijikute tunarudi tulikotoka, Watanzania tushikamane,” alisema.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipongeza hatua ya Rais Magufuli kuunda kamati na kuendesha mchakato wote kwa uwazi huku kila mtu akiona matokeo ya uchunguzi wa kamati.

“Zamani kamati ziliundwa, lakini matokeo ya uchunguzi wa kamati hizo alipewa mtu mmoja. Kwa hiyo wananchi walikuwa hawajui kamati imebaini nini na mapendekezo ya kamati hizo yalikuwa hayafanyiwi kazi,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye alisema kilichomshangaza zaidi ni kampuni kubwa kama Acacia kufanya biashara bila kusajiliwa na Wakala wa Usajili wa Kampuni na Majina ya Biashara (Brela) na kwamba hilo ni somo kwao.

No comments