Breaking News

Sharti la ukazi lazua hofu CCM

Polepole alinukuliwa na Redio Times juzi akisema kuwa wanachama wa CCM wanaotaka kugombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa 2020 wanatakiwa kuwa wakazi wa eneo husika.
 Kauli ya katibu wa uenezi wa CCM, Humphrey Polepole imezua hofu miongoni mwa wabunge wa chama hicho, huku wengi wakisita kutoa maoni yao.
Polepole alinukuliwa na Redio Times juzi akisema kuwa wanachama wa CCM wanaotaka kugombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa 2020 wanatakiwa kuwa wakazi wa eneo husika.
Inakadiriwa kuwa nusu ya wabunge wa CCM hawaishi katika majimbo yao kwani wengi wao wanaishi mijini na hasa Dar es Salaam jambo ambalo linaweza kuwatoa katika mchakato wa kuwania nafasi hiyo miaka mitatu ijayo.
Wengi wa wabunge wa chama hicho walioulizwa kutoa maoni yao kuhusu kauli hiyo ya Polepole waligoma kuzungumza wala kutajwa majina, huku wachache waliokubali kuzungumza wakiwa ‘makini na kauli zao’ jambo ambalo limetafsiriwa kuwa ni kutokana na hofu ya kuogopa kuonekana wasaliti.
Pengine kwa kutoamini msimamo huo wa Polepole, mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe aliuliza kupitia mtandao wake wa twitter, “hpolepole kaka hii ya Times FM kuwa 2020 mbunge lazima awe anaishi jimboni kwake ni kauli yako comrade”.
Ukiondoa swali hilo la Bashe, wabunge wengine hawakuwa tayari kuzungumzia lolote kuhusu msimamo huo wa Polepole kwa madai walikuwa hawajamsikia ‘mwenezi’ huyo wa CCM.
Mbunge wa Songwe, Phillip Mulugo alisema hataweza kuzungumzia suala hilo kwa sababu hakusikia lililozungumzwa. “Sikusikia ilipozungumzwa kwa hiyo sitaeleza chochote,”alisema.
Wakati wabunge wengine simu zao ziliita bila kupokelewa, mbunge wa Jimbo la Manonga, Seif Khamis Gulamali simu yake ilikatika kabla ya kutoa maoni na baadaye haikupatikana
tena.

SIKILIZA AUDIO MAGAZETI YA LEO HAPA

No comments