Breaking News

SETH ANASUMBULIWA NA PUTO LILILOPO TUMBONI

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imeambiwa kuwa ‘puto alilonalo tumboni mfanyabiashara Harbinder Singh Sethi, linamtesa.

Madai hayo yalitolewa mahakamani jana na wakili wa utetezi, Joseph Makandege, kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, ili mshtakiwa aruhusiwe kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

”Mheshimiwa, taarifa za kitabibu dhidi ya mshtakiwa na nyaraka tulishaziwasilisha mahakamani na kwamba anaweza kupoteza maisha endapo uvimbe ulio kama puto tumboni mwake ukipasuka kwa kukosa matibabu,” alidai wakili huyo.

Kutokana na madai hayo, hakimu alitoa amri kwa mara ya pili upande wa Jamhuri kumpeleka Sethi kutibiwa Hospitali ya Muhimbili kama ilivyogiza awali.

Awali, kabla ya amri hiyo, Wakili wa utetezi, Joseph Makandege, alidai upande wa Jamhuri haujampeleka mshtakiwa kupata matibabu Muhimbili kama mahakama ilivyoagiza badala yake wamempeleka Amana.

“Mheshimiwa hakimu, mahakama yako imetoa amri mara mbili ikiuelekeza upande wa Jamhuri kumpeleka  mshtakiwa Hospitali ya Muhimbili baada ya maombi ya upande wa utetezi,” alidai wakili wa utetezi na kuongeza:

“Mshtakiwa wa kwanza ni mgonjwa na kwa maradhi yake anastahili kupata matibabu Muhimbili, nimewasiliana na mshtakiwa nimebaini kuwa kilichofanyika si sahihi badala yake Magereza wamempeleka hospitali wanayoijua wao…kilichofanyika ni kinyume cha amri ya mahakama kifungu cha 53, kifungu kidogo cha (1) kinatoa fursa kwa mtu yeyote aliyeko ndani kama anaumwa kufikishwa hospitali ili apate matibabu.”

Alidai pamoja na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ina jukumu la kuhakikisha tararibu za kisheria zinafuatwa na haki inatendeka.

Aliendelea kudai ni rai yao kuwa mshtakiwa apelekwe Muhimbili ili kuhakikisha afya yake inazingatiwa na kuhifadhiwa ili aweze kuhudhuria mashtaka dhidi yake.

Akijibu hoja za utetezi, Wakili wa Serikali, Vitalis Peter, alikiri kifungu cha 53 kinaipa mamlaka Magereza kumpeleka mtuhumiwa hospital kama anaumwa na Magereza wana wataalamu wao na hospitali yao.

Alisema wataalamu hao ndio wanakaa na mtuhumiwa na wanamuangalia kwa mara ya kwanza na wakishindwa kumtibu ndipo wanampa rufani kwingineko.

Vitalis alidai mshtakiwa alihudumiwa na wataalamu wa Magereza na baadaye walimpeleka hospitali ya juu ambayo ni Amana.

“Mshtakiwa alipatiwa matibabu katika Hospitali ya  Amana na daktari bingwa kutoka Muhimbili, Dk. Wilson Mgamba, ambaye alimuona mtuhumiwa na kujiridhisha na afya yake,” alidai wakili Vitalis.

Alidai Magereza walimpeleka hospitali na kwa mujibu wa taratibu zao hawapangiwi hospitali ya kumtibu mtuhumiwa.

Naye mshtakiwa wa pili, mfanyabiashara James Rugemalira, aliiomba mahakama kumpa kibali cha kuonana na mawakili wake kwa sababu ana mambo mengi ya kuongea nao.

Alidai ana mawakili 10 na kuna wakati anahitaji kuongea nao, lakini ana uwezo wa kuwaona wawili tu, hivyo anaomba kupatiwa dakika 30 kuzungumza nao kabla hajarudishwa mahabusu.

Hakimu Shahidi alikubali ombi la Lugemalira na kuwaagiza Magereza kushughulikia tatizo hilo. Kesi hiyo itatajwa Septemba 14, mwaka huu.

Katika kesi ya msingi, Seth na Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa VIP Engineering LTD na mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi  kwa kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani milioni 22. 1 na Sh. bilioni 309 pamoja na utakatishaji fedha.

Inadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Ilidaiwa katika mashtaka ya pili kati ya Oktoba 8,2011 na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam wakiwa siyo watumishi wa umma walishirikiana na watumishi wa umma  kutekeleza  mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika mashitaka ya tatu yanayomkabili Sethi, inadaiwa  Oktoba 10, 2011 katika mtaa wa Ohio Ilala Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai, alighushi fomu namba 14 A ya usajili wa Kampuni  na kuonyesha ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua sio kweli.

Pia, Seth anadaiwa alitoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14 A ya usajili wa kampuni kwa Ofisa msajili wa Kampuni, Seka Kasera kwa njia ya kuonyesha ni Mtanzania na mkazi wa Mtaa wa Mrikau, Masaki Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Aidha, ilidai katika mashtaka ya kujipatia fedha kwamba  kati ya  Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika Makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni  na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph,  kwa ulaghai walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dola za Marekani  22,198,544.60 na Sh za Kitanzania 309, 461,300,158.27.  

Pia washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la  kati Kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh  309,461,300,158.27.

Kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dola za Marekani milioni 22.1 na Sh. bilioni 309.4  wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Pia alidai Novemba 29,2013 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Tanzania Sethi alitakatisha fedha kwa kuchukua kutoka BoT, dola za Marekani milioni 22.1 wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Aidha, Sethi anadaiwa kati ya Novemba 29, 2013 na Machi 14,2014 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Kinondoni Dar es Salaam alitakatisha fedha, Sh. bilioni 309.4  kutoka BoT wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao uhalifu.

Katika mashtaka ya 10,  inadaiwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi tawi la St. Joseph Cathedral, Rugemalira  alitakatisha fedha, ambazo ni  Sh. bilioni 73.5 kutoka kwa Seth wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Kadhalika, inadaiwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi tawi hilo, Rugemalira alitakatisha dola za Marekani 22,000,000 kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo ni zao la uhalifu.

Sethi anadaiwa Januari 28, 2014 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic wilaya ya Kinondoni alihamisha Rand 1,305,800 za Afrika Kusini kwenda kwenye akaunti namba 022655123 katika Benki ya Standard Land Rover Sandton ya Afrika Kusini  wakati akijua katika kipindi anahamisha fedha hizo zimetokana na zao la kujihusha na genge la uhalifu.

No comments