TAKUKURU Yawafikisha Mahakamani Vigogo Watano wa TANESCO
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu vigogo watano wa zamani wa Shirika la Umeme Tanzania, Tanesco wakidaiwa kuhujumu uchumi kwa kuisabishia Serikali hasara ya Tsh. Milioni 275.
Waliofikishwa Mahakamani ni pamoja na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Robert Shemhilu, Ofisa Ugavi, Harun Mattambo, Mkurugenzi wa Fedha, Lusekelo Kasanga, Mwanasheria wao, Godson Makia pamoja na msambazaji kutoka kampuni ya M/S Young Dong Electronic Co. Ltd Martin Simba.
Wakili wa Serikali, Vitalis Peter aliwasomea washtakiwa hao mashtaka mawili ya uhujumu uchumi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba ambapo alidai kuwa kati ya January na December 2011 katika Ofisi za Tanesco Ubungo, washtakiwa wakiwa waajiriwa wa Shirika hilo, walitumia madaraka yao vibaya kwa kufanikisha malipo kwa msambazaji Martin Simba bila ya kufanya uhakiki.
Aidha, Wakili Vitalis amedai kati ya January na December 2011 katika Ofisi za Tanesco Ubungo, washtakiwa hao wakiwa waajiriwa wa shirika hilo pamoja na msambazaji huyo waliisababishia Serikali hasara ya Tsh. Milioni 275.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa waliruhusiwa kuongea kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka DPP amewasilisha Cheti maalum kinachoiruhusu Mahakama kuisikiliza kesi hiyo ambapo walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi umekamilika.
Hakimu Simba aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja alisaini bondi ya Tsh. Milioni 40 huku mmoja kati ya wadhamini hao akitakiwa kuwasilisha hati ya Mali isiyohamishika ambapo walitimiza masharti hayo.
Washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali (PH) August 24, 2017.
No comments