Breaking News

Kesi ya Lema kusikilizwa kwa maandishi

Mahakama kuu kanda ya Arusha leo  imeahirisha rufaa iliyokatwa na mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema ya kupinga  uamuzi  wa kesi ya kusambaza ujumbe kwa njia ya video wa kuhamasisha maandamano  ya Septemba mosi mwaka 2016 yaliyojulikana kwa jina la UKUTA.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo kutokana na upande wa Jamhuri kudai kutokuwa na taarifa (nakala) kuhusu shauri hilo.

Mbele ya mahakama kuu wakili wa serikali, Innocent Njau aliiomba mahakama kuendelea kusikiliza kesi hiyo wakati wakifuatilia hati ya wito wa mahakama ambayo wamedai hawakuwa wamepatiwa na kwamba siku ya leo walikuwepo mahakamani hapo kwa ajili ya kesi nyingine.

Wakili anayemuwakilisha mbunge huyo, Sheki Mfinanga amesema kutokana na hali hiyo wameiomba mahakama kuahirisha shauri hilo lakini hata hivyo mahakama kupitia kwa jaji Dkt. Modesta Opiyo iliamua kukubaliiana na ombi la upande serikali la kutaka shauri hilo kusikilizwa kwa njia ya maandishi.

Jaji Opiyo amepanga tarehe 30 mwezi Agosti kuwa ni siku ya mawakili wa Lema kuwasilisha hoja zao na baadaye tarehe 13 mwezi Septemba mwaka huu upande wa serikali utawasilisha hoja zao kabla ya kuwasilishwa kwa hoja za ziada tarehe 20 mwezi Septemba mwaka huu.

Baada ya kutoa maelekezo hayo jaji Opiyo aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 27 mwaka huu kwaajili ya kupanga tarehe ya kutoa uamuzi.

No comments