Hakimu wa wilaya Mtwara ashambuliwa kwa mapanga
Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Halfani Ulaya, amejeruhiwa vibaya sehemu za mwili na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi akiwa nyumbani kwake usiku wa kumkia Jumanne.
Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Neema Mwanga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea Jumatatu usiku wa 2:30 wakati hakimu huyo akiwa amelala nyumbani kwake maeneo ya Mtandi Kata ya Mtandi.
Kamanda Mwanga alisema watu watatu wakiwa na mapanga walivamia nyumba ya hakimu huyo kisha kuanza kuwasumbua watoto wake ambao walikuwa nje ya nyumba hiyo, na baada ya Ulaya kusikia sauti za watoto wake alitoka nje na kukutana na majambazi hao.
Alieleza wakati Ulaya akiwa katika jitihada za kuwaokoa watoto wake wakiwa mikononi mwa majambazi hao, walianza kumpiga kwa mapanga hayo na kumjeruhi katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Alisema Hakimu huyo amejeruhiwa sana katika maeneo ya mikono. Lakini alifanikiwa kukimbia na majambazi hao walifanikiwa kutoroka bila kuchukua chochote.
Alisema hadi sasa hakuna anayeshikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na atakayebainika kuhusika na hili atafikishwa katika mkono wa sheria.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hispitali hiyo, Dk. George Kumwembe, alithibitisha kumpokea hakimu huyo akiwa na majeraha na kupatiwa matibabu ya awali.
Dk. Kumwembe alisema kuwa hakimu huyo amepatiwa rufaa kwenda Hospitali ya Peramiho, Songea kutokana na hali yake kutokuwa ya kuridhisha.
No comments