Shamrashamra za CCM zazima baada ya JPM kutoa onyo hili
Tishio la mwenyekiti wa CCM, John Magufuli la kukata majina ya wagombea watakaotumia rushwa katika uchaguzi, limesababisha hofu na kufanya uchaguzi wa ngazi za chini kukosa msisimko.
CCM inaendelea na uchaguzi wa viongozi wake wa kuanzia ngazi ya mashina na matawi na katika baadhi ya mikoa uchaguzi uko ngazi ya katanchini kote. Watakaochaguliwa watashika nyadhifa hizo hadi 2022.
Hata hivyo, uchaguzi huo unaonekana kukosa msisimko kama ilivyozoeleka na uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa onyo la Rais Magufuli limerudisha nidhamu ndani ya chama.
Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuwa chama hicho kilikuwa kimetekwa na matajiri na ndio waliokuwa wanaaamua nani awe kiongozi kutokana na nguvu yao ya fedha.
Kabla na hata baada ya kuchaguliwa kuwa Rais mwaka 2015, na baadaye mwenyekiti wa chama hicho, Dk Magufuli aliapa kupambana na rushwa na kuahidi kuirudisha CCM kwa wanachama.
Onyo la Magufuli lilikuwaje?
Akifunga semina ya viongozi na watendaji wa CCM ngazi ya wilaya na mkoa mjini Dodoma Machi 14 mwaka huu, Rais Magufuli aliapa kukata majina ya wagombea watakaotumia rushwa.
“Tusikubali rushwa, na nitafuatilia kwelikweli. Na wa kufuatilia wako wengi. Watakaotumia rushwa kuomba nafasi zao hawatarudi,” alisema Rais Magufuli katika ufungaji huo wa semina hiyo.
“Uwe ulikuwa mwenyekiti wa zamani au mgombea mpya hutarudi. Wewe chukua fomu yako wala usijali waache watakaotoa rushwa watumie. Hata awe wa kwanza kamwe hatarudi.
“Hili nataka niwaeleze ukweli kwa sababu nisiposema ukweli hatuwezi (kuendelea). Tukajenga chama cha watoa rushwa. Yeyote atakayetoa rushwa ili ashinde uchaguzi nasema jina halitarudi.”
Viongozi, wanachama wanena
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti kuhusu uchaguzi unaoendelea, viongozi na wanachama wa CCM walisema onyo hilo la Rais Magufuli limesaidia kurudisha nidhamu ndani ya chama hicho kikongwe barani Afrika.
Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo alisema onyo la mwenyekiti wao limesaidia kurudisha nidhamu ya uchaguzi huo na ushindani sasa utakuwa ni wa sifa na si fedha.
“Ule utaratibu wa kusema sijui natangaza nia siku kadhaa nyuma kabla ya kuruhusiwa, haupo tena. Hii ndiyo ilikuwa inatuletea shida maana watu walikuwa wanaunda mpaka mitandao yao,” alisema.
Tarimo alisema hivi sasa vile vikao visivyo rasmi vilivyokuwa vikifanyika katika mabaa na ofisi za wagombea kuelekea kwenye uchaguzi havipo tena kwa vile kila mtu anaogopa kutumbuliwa.
“Kwa kweli nidhamu imerudi na wewe tazama hata viongozi safari hii watakaopatikana utakuta ni wale ambao kweli wana uchungu na chama sio wale wanaotafuta njia ya kupata masilahi,” alisema.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoaani Kilimanjaro, Juma Raibu alisema mabadiliko ya utaratibu ndani ya chama yameondoa kampeni chafu mitaani.
“Sasa hakuna mtu anayejua jina lake litarudi ama la na utaratibu ni kuwa majina yaliyorudi yatatangazwa palepale ukumbini. Hilo limewafunga wengi mikono. Hakuna rafu tena,” alisema.
Mwenyekiti huyo ambaye anamaliza muda wake na kwa sababu ya umri hatagombea tena nafasi hiyo, alisema hivi sasa hakuna aliye tayari kufanya shamrashamra wakati hana uhakika wa jina kurudi.
“Huko nyuma unakuta wanajitokeza wagombea 10 wanatangaza nia wanaingia mitaani, wanafanya wanayoyajua. Sasa hivi ole wake mtu atoe rushwa hata ya shilingi moja jina lake halitarudi,” alisema.
Akizungumza na wanahabari juzi alipokuwa akitangaza UVCCM kuanza kutoa fomu kuanzia jana, Raibu alisema hata wagombea watakaochafua na kukashifu wagombea wenzao, majina yao yataondolewa.
“Hao wanaopenda kuchafua wenzao kama njia ya kuwaharibia safari, hakuna hiyo njia tena. Wote wataomba kura sehemu moja na tukikubaini unachafua wenzako mitaani jina halirudi,” alisema.
Kada wa chama hicho aliyeomba jina lake lisitajwe, alisema awali mambo yalikuwa shaghalabaghala kiasi kwamba wakati wa uchaguzi kulikuwa kunaibuka wanachama feki wasiojulikana.
“Walikuwa wananunulia watu kadi na kuzilipia miaka mingi mbele ili tu waje awmchague. Sasa hivi thubutu yake wafanye hivyo watausikia uongozi kwenye redio. Magufuli ni mwanamume,” alisema.
Kada huyo alisema siku kama hizi miaka ya 2002, 2007 na 2012, ilikuwa ni kipindi cha mavuno kwa wanachama wa CCM kutokana na utamaduni uliokuwa umezoeleka wa kupewa fedha na wagombea uongozi.
“Lakini sasa hivi huoni hayo mambo. Maana hujui ni watu gani watatumwa kufuatilia maana Rais alisema wako wengi wa kufuatilia. Sasa wewe gawa pombe toa rushwa uone moto wake,” alisema.
No comments