Breaking News

Mtu Mmoja Afariki na wengine Kujeruhiwa kwenye Ajali, Lindi



Mtu mmoja amefariki, na wengine wengi kujeruhiwa kutokana na ajali ya basi iliyotokea jana jioni katika eneo la Kinyope wilaya ya na mkoa wa Lindi. 

Habari ambazo bado hazijathibitishwa  na mamlaka husika, ikiwamo jeshi la polisi na uongozi wa hosipitali ya rufaa ya mkoa wa Lindi ya Sokoine zimeeleza kwamba ajali hiyo ambayo imesababisha mtu mmoja kufariki na wengine kujeruhiwa ilitokea jana jioni baada ya basi linalotambulika kwa jina la Rondo best kupinduka katika kijiji cha Kinyope kata ya Rutamba, baada ya kushindwa kupanda mlima. 


Rondo best ambalo bado namba zake za usajili wala jina la dereva  havijafahamika lilikuwa linatoka Lindi kwenda Milola. Baadhi ya ndugu na jamaa wa waliopata ajali waliokuwepo katika hosipitali ya Sokoine iliyopo katika manispaa ya Lindi walisema watu wengi wamejeruhiwa, ambao walikuwa wanaendelea kuletwa katika hosipitali ya Sokoine walikuwa wanatolewa kutoka katika zahanati ya Rutamba na kituo cha afya cha Milola ambako walikimbizwa baada ya kutokea ajali hiyo katika eneo hilo ambalo linatajwa kuwa na mlima na mteremko mkali. 


Hadi sasa mtu mmoja  amefariki, lakini watu wengi wamejeruhiwa na wengine hali zao ni mbaya sana. Kama unavyoona ajali imetokea jioni, lakini wanaendelea kuletwa hadi usiku huu, "alisema mmoja wa watumishi wa hosipitali ya Sokoine ambae hakutaka jina lake litajwe kutokana na kuwa sio msemaji wa hosipitali hiyo. Hadi habari hii inaandikwa majeruhi walikuwa wanaendelea kupelekwa katika hosipitali hiyo. Taarifa kamili mtaletewa baada ya mamlaka husika kupata wasaa na utulivu wa kuweza kutoa nafasi ya kueleza

No comments