Breaking News

Mbunge Anusururika Kichapo Bungeni


JULIANA Shonza, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) amenusurika kuangushiwa kipigo kikali na wabunge wa Chadema mara baada kuwatambia kuwa atahakikisha Halima Mdee, Mbunge wa Kawe (Chadema), anaendelea kukaa nje ya Bunge kwa mwaka mzima, 

Tukio hilo limetokea leo katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma ambapo Shonza alisikika akisema atapeleka hoja bungeni ili adhabu ya Mdee kutohudhuria vikao vya bunge iongezewe. 

Itakumbukwa kuwa Mdee na Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini wamefungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda wa mwaka mmoja huku adhabu hiyo ikipingwa vikali ambapo tayari Bulaya na Mdee wamefungua kesi mahakamani kupinga. 

Suzan Kiwanga, Mbunge wa Jimbo la Mlimba (Chadema) ambaye alikuwa karibu na Shonza ambapo alimtaka mbunge huyo kuacha siasa za chuki na roho mbaya kwani hata Mdee akikaa nje ya bunge hatofaidika na lolote. 

“Acha roho mbaya. Wewe ni mwanamke, unafurahia vipi mwenzako akipata matatizo? Kukaa kwake nje hakuwezi kukusaidia kitu na kumbuka malipo ni hapa hapa duniani,” alifoka Kiwanga. 

Kauli ya Kiwanga iliamsha hasira za Shonza ambaye alianza kumtolea maneno machafu yasiyofaa kuandikwa gazetini. Ndipo baadhi ya wabunge wa Chadema waliokuwa jirani akiwemo Pauline Gekul, Mbunge wa Babati Mjini na Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, wakamvaa na kumtaka awe heshima kwa kuangalia umri wa mbunge aliyekuwa akimtolea maneno machafu. 

Shonza hakutaka kuwaelewa wabunge hao, aliendelea kukabiliana nao huku akifoka kwa hasira na ghafla akaanza kuangua kilio ndipo Tweve na Zainab Vullu, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), wakamvuta na kumtoa nje ya geti la Bunge akipiga kelele zilizoambatana na kilio. 

“Niacheni, Niacheni…..kama wanataka kunipiga waacheni wanipige tu.. niacheni niacheni,” alizungunza Shonza huku akijitahidi kujivuta kutoka mikononi mwa wabunge wa CCM waliokuwa wanamvuta. 

“Mhe. Vullu hebu mfunzeni adabu huyu binti, huenda ana matatizo makubwa ya akili, haiwezekani anawatolea maneno machafu watu wazima huku akitaka kupigana nao, hii ni aibu. Huyu binti mnamuangalia tu wakati anaharibikiwa,” amesema Gekul. 

Upendo Peneza, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) ambaye alikuwepo katika eneo hilo alisema “Tatizo Shonza anapenda kukurupuka. Anatia aibu sana, binti mdogo anataka kupigana na watu mtu mzima mwenye umri wa mama yake.” 

No comments