Kauli ya Rais Magufuli yamuibua Tundu Lissu
Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amesema kitendo cha Rais John Magufuli kuwataka wafunge midomo ni kuminya haki ya watu kutoa maoni yao.
Kauli hiyo ya Lissu imekuja siku moja baada ya juzi, Rais Magufuli kusema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakishinikiza Serikali kuwaondoa gerezani watu wanaoshikiliwa na polisi na akawaonya wanaofanya hivyo kufunga midomo.
Hivi karibuni, waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa alikaririwa akitaka kuachiwa huru kwa masheikh wa taasisi ya Uamsho akisema wamekaa ndani kwa muda mrefu bila kuhukumiwa.
Kauli hiyo ilisababisha Lowassa aitwe Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano ili chombo hicho cha dola kione kama maneno yake yana mwelekeo wa uchochezi au la.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu kauli ya Rais Magufuli, Lissu alisema wananchi wana haki ya kuhoji viongozi hao wa dini wanaoendelea kukaa mahabusu bila kuhukumiwa.
Alisema wanasiasa watamkosoa Rais kama ataminya uhuru wao wa kutoa maoni bila kuvunja sheria.
Aliungwa mkono na Anna Henga ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), aliyesema kisheria hakuna kosa kuhoji ikiwa mtu anakaa muda mrefu mahabusu bila kuhukumiwa.
“Si kosa kwa wananchi kuhoji kama wanaona ndugu au jamaa zao wamekaa mahabusu bila kuhukumiwa, ni wajibu wao kuhoji,” alisema Henga ambaye pia ni mwanasheria.
Alisema wananchi wana haki ya kuuliza kwenye mamlaka husika kuhusu mienendo ya kesi zinazowahusu ndugu na jamaa zao.
“Kwa hiyo wanatakiwa kuelewa sababu zinazochelewesha kutolewa kwa hukumu za ndugu ama jamaa zao, hii ni haki yao,” alisema.
Alisema hata wanasiasa wanaozungumzia kuhusu watu walioko mahabusu wana haki ya kufanya hivyo.
No comments