Breaking News

FIFA YASITISHA KUJA TANZANIA


 

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limefuta mpango wake wa kutuma wawakilishi wake nchini Tanzania kwa ajili ya kufuatilia mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Taarifa hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa TFF ambaye pia ndiye anayekaimu nafasi ya Rais wa TFF, Wallace Karia ambaye amesema kuwa FIFA wamefikia uamuzi huo kutokana na mazungumzo waliyoyafanya na TFF kwa njia ya simu, pamoja na taarifa zilizotumwa katika shirikisho hilo kutoka Tanzania.

Karia amesema katika mazungumzo hayo amewaeleza kila kitu kinachoendelea nchini, na kwamba leo,Jumanne Kamati ya Utendaji inakutana, jambo ambalo limewaridhisha na kuitakia kila la kheri kamati hiyo ya utendaji katika kikao chake cha leo.

“FIFA hawatakuja tena, tuliongea nao tukawaeleza kinachoendelea, walitupigia wakitaka kujua kama kulikuwa na muingilio wa serikali katika mchakato, au kama kuna pesa za FIFA zilizotumika vibaya, tukawaambia siyo kweli na kuwaeleza kilichotokea kwahiyo hawatakuja,” amesema Karia.

Kuhusu kikao cha leo cha kamati ya utendaji, Karia amewataka wadau wa soka nchini wakiwemo wagombea kuwa watulivu na kuiamini kamati hiyo kwani itakuja na uamuzi mzuri na wenye afya kwa mpira wa Tanzania.

Kikubwa kitakachojadiliwa katika kikao hicho ni hatma ya Kamati ya Uchaguzi ambayo wajumbe wake wameshindwa kuelewana na huenda ikapanguliwa ili kuruhusu uchaguzi uendelee.

@AzamTV

No comments