Breaking News

Chadema Arusha yataka wanaotaka kuhama chama waondoke haraka

Hadi sasa madiwani watano wa Chadema mkoani hapa wameshajiondoa. Madiwani hao ni Credo Kifukwe (Murieti), Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Greyson Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu (Viti Maalumu).

 Chadema mkoani Arusha imewapa mkono wa kwaheri viongozi wake wanaotoka kuhama na kuwataka waondoke sasa kwa kuwa chama hicho “kitakuwa na kazi kubwa ambazo zitahitaji kujitoa kwa dhati”.

Hadi sasa madiwani watano wa Chadema mkoani hapa wameshajiondoa. Madiwani hao ni Credo Kifukwe (Murieti), Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Greyson Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu (Viti Maalumu).

Katika taarifa aliyoitoa jana kuhusu wimbi la kujiuzulu kwa madiwani, mwenyekiti wa Chadema wa mkoa, Aman Golugwa alisema kuondoka kwao hakuathiri chama hicho.

“Wana Chadema msisikitike, wamechelewa kuondoka na msione kuwa wanatushtukiza, hapana. Wao ndio wamekaa kwa mateso na sasa hawana budi kuondoka maana hawakuwa wa kwetu,” alisema.

Golugwa alisema bado kuna watakaoondoka na kwamba chama hicho hakitawazuia kwa kuwa kilijua kuna watu wataondoka na baadhi bado wapo njiani.

“Tuwaache waondoke wenyewe. Kazi iliyopo mbele yetu ni kubwa na inahitaji waliojitoa hasa na wenye mapenzi mema na nchi hii kwa kuwa hila yao kwa kipindi walichokaa nasi na dhambi yao ya maneno ya uongo wakati wa kuondoka kwao, watailipa tu,” alisema.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kujiuzulu kwa madiwani wa chama hicho katika kata hizo kunatokana na ushawishi wa fedha na madaraka, jambo ambalo limekanushwa na madiwani hao.

Katika taarifa walizotoa baada ya kujiuzulu, madiwani hao wamekuwa wakieleza kuridhishwa kwao na utendaji wa Rais John Magufuli na wasaidizi wake na hivyo kusema hawana sababu ya kupingana na Serikali iliyopo madarakani.

Katika uchaguzi uliopita, Chadema Mkoa wa Arusha ilifanikiwa kushinda majimbo sita kati ya saba na kuongoza halmashauri tano kati ya saba jambo ambalo halijawahi kutokea.

No comments