Mjadala wa wanafunzi kupata mimba wakiwa shule wakolea
Dar es Salaam. Kauli ya Rais John Magufuli kuwa hakuna mwanafunzi atakayeendelea na shule baada ya kujifungua, imepokewa kwa hisia tofauti.
Wanaharakati, wadau wa elimu na wabunge wanaipinga kauli ya Rais huku ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ikitofautiana na msimamo wa kiongozi huyo wa nchi.
Wapo wanaotaka wanaopata mimba shuleni wapewe fursa ya kuendelea na elimu na wengine wamempongeza Rais wakisema kuzuia kuendelea na masomo katika shule za Serikali kutapunguza mimba za utotoni.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akizindua Barabara ya Bagamoyo – Msata mkoani Pwani na kusisitiza kwamba katika utawala wake, hakuna mwanafunzi yeyote mwenye mtoto atakayeruhusiwa kurudi shuleni kwa sababu Serikali inatoa elimu bure kwa watoto na si wazazi.
Kutokana na maudhui ya shughuli ya uzinduzi wa barabara, haikutegemewa kama Rais Magufuli angetoa msimamo huo mkali, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inatafuta mbinu za kusaidia wasichana wanaopata mimba shuleni kutokana na baadhi yao kupata ujauzito kwa kubakwa, mazingira magumu ya shule, hasa vijijini na wengi wao kutokana na umaskini.
Rais alitoa kauli hiyo wakati akizungumzia wafungwa wanaoishi kwa starehe gerezani, akiagiza wafanye kazi ya kulima, kama hao wanaowapa mimba wanafunzi na kutakiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.
Hata hivyo, Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, inaitaka Serikali kuweka mazingira ya kuwezesha wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo.
“Wasichana wote wa elimu msingi, wanaoacha shule kwa sababu ya kupata ujauzito, wataendelea na masomo,” inasema ilani hiyo.
Lakini Rais alisema wanaotaka wasichana hao waendelee na masomo waanzishe shule zao za wazazi.
Akizungumzia kauli hiyo, mtaalamu wa saikolojia kutoka Kituo cha Afya ya Akili cha Mehota, Dk Bonaventura Bagile alisema mwanafunzi aliyewahi kubeba mimba anaporudi shule anajenga picha mbaya kwa wanafunzi wenzake.
Alisema wanafunzi wanafundishwa kutofanya mambo fulani wakiwa shuleni, lakini wakiona mwenzao kafanya mambo hayo na bado amerudi shule, hawatakuwa na nidhamu kwa sheria na kanuni zinazowaongoza.
“Mwanafunzi mzazi akiruhusiwa kurudi shule, itajenga image (taswira) mbaya kwa wenzake kwamba you can do something bad and there are no consequences (unaweza kufanya jambo baya na usipate matokeo yoyote),” alisema mtaalamu huyo.
Dk Bagile aliunga mkono kauli ya Rais Magufuli akisema mtu anapofanya jambo baya, lazima ajue kwamba kuna matokeo fulani atakabiliana nayo na mengine yanaweza kumgharimu maisha yake.
Kauli hiyo iliungwa mkono na katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Kigoma, Jackson Gaima ambaye alisema mtoto akipata mimba wakati akiwa shuleni anakuwa amevunja kanuni na maadili ambayo hayaruhusu wanafunzi kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi.
“Kuna kesi za ubakaji kweli, lakini suala hilo lisiwe ndiyo ajenda ya kuhalalisha wanafunzi kubeba mimba na kurudi shule,” alisema Gaima.
“Serikali iweke utaratibu maalumu wa kushughulikia masuala ya ubakaji na kuwaangalia kipekee watoto wanaopata mimba kwa kubakwa.”
Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya HakiElimu, John Kallaghe alisema wameipokea kauli ya Rais Magufuli na kwamba watatafuta nafasi ya kuzungumza naye ili wamueleze ni kwa nini wanapigania watoto kurudi shule baada ya kujifungua.
Kallaghe alisema ripoti mbalimbali za utafiti zinaonyesha kwamba zaidi ya watoto 70,000 wanashindwa kuendelea na masomo kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mimba za utotoni, jambo linaloonyesha kwamba kuna tatizo.
“Tunaamini kwamba kupata mimba si mwisho wa mtoto kuendelea na masomo. Leo (jana) wadau wa elimu tutakutana kwa ajili ya kujadili suala hilo. Ninaamini tutatoka na kauli moja,” alisema mkurugenzi huyo wa taasisi ambayo imekuwa ikipigania wanafunzi waliojifungua waruhusiwe kuendelea na masomo.
Wabunge Ukawa waja juu
Mjadala wa msimamo huo wa Rais pia ulitawala kwa wabunge huku wale wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakipinga kwa maelezo kwamba kuruhusu hali hiyo ni kukiuka mikataba ya kimataifa na Katiba.
Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Suzan Lyimo alisema jana kuwa watoto wote wana haki sawa ya kupata elimu kikatiba.
“Mimi kama mzazi nilisikitishwa sana na kauli ile. Muda mrefu sana tumekuwa tukitetea elimu ya watoto wetu. Taasisi mbalimbali zimezungumza kuhusu jambo hili,” alisema.
Alisema pia ipo nyaraka ya Serikali ya jinsi gani watoto wanaopata mimba wanavyoweza kurudi shuleni na kwamba Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Stella Manyanya akijibu swali katika vikao vya Bunge vya Februari aliwaambia kuwa mwongozo wa jambo hilo unaandaliwa.
Alisema suala hilo lilirejea katika Bunge la Bajeti wakati Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambayo yeye ni mjumbe, ilipolizungumza katika maoni yake.
Alisema Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kufanya jambo hilo akisema hata Zambia na Kenya zinafanya utaratibu huo.
“Sisi kama nchi tumesaini mikataba mbalimbali ya haki za mtoto, vilevile tuna Sheria ya Mtoto na tumesaini mikataba mbalimbali,” alisema.
Alisema jambo alilolifanya Rais Magufuli linakwenda kinyume na maazimio waliyoyasaini.
Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Upendo Peneza alisema mara kadhaa amekuwa akizungumzia umuhimu wa kuwapo kwa elimu ya uzazi shuleni ili kuwezesha watoto wa kike kutambua miili yao na wakati gani kushiriki vitendo vya ngono.
“Watu wengi elimu hii wanaichukulia kuwa inaweza kuwa kichocheo cha kufanya haya mambo, lakini si kweli,” alisema Upendo.
Alisema kuwa Rais alisema kuwa watoto wanaopata mimba waende Veta lakini katika vyuo hivyo vya ufundi hawachukui mtoto ambaye hajamaliza kidato cha nne.
“Kwa lugha nyingine unawaambia wasipate elimu ya shule ya msingi, sekondari wala Veta,” alisema.
Mbunge wa Buyungu (Chadema), Kasuku Bilago alisema hivi sasa hali ni ngumu na inawalazimu watoto kusafiri umbali mrefu kwenda shule na wakiwa njiani wanakumbana na vishawishi.
Alisema waliwahi kwenda Zambia na kujionea jinsi utaratibu wa watoto wanaopata mimba kurejea shuleni unavyotekelezwa.
Alisema utaratibu huo umefanikiwa na umepunguza mimba kwa kiasi kikubwa kwa wanafunzi wanaporudi shule kuona aibu na kuwafanya wenzao kujichunga.
Wasemavyo wengine mitandaoni
Baadhi ya wanasiasa na watu maarufu pia wametoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii huku wakionyesha tofauti zao za misimamo kuhusu kauli ya Rais Magufuli ambayo imekuwa gumzo nchini.
Katika akaunti yake ya Twitter, mbunge wa Kigoma Mjini, Zito Kabwe ameandika: “Ni marufuku mtu yeyote au mamlaka yeyote kubagua mtu mwingine chini ya sheria yeyote au katika utendaji wowote wa dola – Katiba JMT 13(4)(5).”
Aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimri), Dk Mwele Malecela ameandika pia ameandika: “Mama Kamm ni mwanamke jasiri aliyetafuta njia za kuhakikisha watoto wa kike wanasoma baada ya kupata ujauzito na Baba wa Taifa alijua hilo.”
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ameandika: “Anayeamini kila mtoto aliyepata mimba amefanya uhuni anatakiwa kunyimwa fursa!! Ni janga kubwa sana!”
Mkurugenzi wa taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi ameandika:“Naamini elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana ni suluhu ya muda mrefu. Ila wale wanaojikwaa pia ni muhimu tuweke mifumo ya kuwapokea.”
No comments