Breaking News

Wakuu wa mikoa 11 watoa tamko hili kwa JPM

Singida. Wakuu wa mikoa 11 wamempongeza Rais John Magufuli kwa kazi kubwa, nzuri na ya kizalendo anayoendelea kuifanya ya kutetea na kulinda rasilimali za nchi kwa masilahi ya Watanzania. 

Wakuu hao ni kutoka mikoa ya  Singida, Rukwa, Katavi, Kagera, Tabora,Dodoma, Manyara, Geita, Shinyanga, Mwanza na Kigoma. 

Wametoa tamko hilo   jana Ijumaa ( Juni 23) kwenye mkutano wa kawaida wa ujirani mwema katika mikoa hiyo ambao  ulifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa. 

Mwenyekiti wa mkutano huo, alikuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry. 

“Sisi wasaidizi wake (Rais Magufuli) tutaendelea kutekeleza na kuzingatia maelekezo katika utendaji wetu wa kila siku.

Aidha, wakati wote tutakuwa pamoja na wananchi na kuwatumikia kwa kutimiza wajibu wetu kwa uaminifu, uadilifu na tutahakikisha masilahi ya wananchi na Taifa yanapewa kipaumbele cha kwanza,” limesema tamko hilo. 

Pia, wakuu hao wa mikoa wametoa wito kwa wananchi na wawekezaji halali wa ndani na nje ya nchi, wamuunge mkono Rais Magufuli kwa kufanya kazi na wakati wote wazingatie sheria za nchi. 

“Tutumie fursa nyingi zinazoendelea kutengenezwa kwa hatua hizo za kizalendo anazochukua mheshimiwa wetu Rais Magufuli.  Kwa mafanikio, maendeleo na tija kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati na uchumi wa viwanda,” limeongeza tamko hilo. 

Mkutano huo wa aina yake kufanyika mjini hapa umesisitiza kwamba kuna haja ya kumtia moyo Rais Magufuli ili aendelee na ujasiri wake huo wa kulinda rasilimali za nchi. 

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa mkutano huo, Mwanry amesema pamoja na mambo mengine wametumia fursa hiyo kubadilishana uzoefu na wamekubaliana kupeana taarifa mbalimbali za kimaendeleo.

 “Tumekutana hapa kwa mapenzi ya nchi yetu na ya Rais wetu Magufuli. Tuliokutana leo hii, changamoto za mikoa yetu zinafanana. Changamoto hizi ni pamoja na uharibifu wa mazingira, uhaba wa mvua, kilimo cha kuhama hama na uhamiaji haramu,” amesema Mwanry na kuongeza; 

“Kwa hiyo tukiacha kila mkoa utatue changamoto hizi kivyake, hatutafanikiwa kizitatua.Tumekubaliana kukutana mara kwa mara ili changamoto zinazotukabili sote tuzipatie ufumbuzi wa kudumu kwa pamoja.” 

No comments