Marufuku biashara ya mahindi mabichi - RC
Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe amepiga marufuku uuzaji wa mahindi mabichi akidai kuwa unaweza kusababisha njaa.
Dk Kebwe amesema kama hakutakuwa na udhibiti wa biashara ya mahindi mabichi kiasi cha chakula kinachotarajia kuvunwa hakitafika na hivyo mkoa unaweza kuingia kwenye aibu ya kuomba chakula kutokana na kukumbwa na njaa.
Kutokana na hilo amewataka wakuu wa wilaya pamoja na watendaji wa kata na vijiji kusimamia biashara hiyo ya mahindi mabichi inayofanywa na wakulima kwa tamaa ya kupata pesa haraka bila ya kuweka akiba ya chakula.
Katika hatua nyingine Dk Kebwe amepiga marufuku matumizi ya nafaka kwa ajili ya kutengeneza pombe kwa sababu zimekuwa zikichangia upotevu wa chakula usiokuwa wa lazima.
Amewataka wenyeji wa mkoa wa Morogoro kuuza kiasi kidogo cha chakula kwa ajili ya kufanya maendeleo na si kucheza ngoma za ‘vigodoro’.
Amesema kuwa wakulima mkoa wa Morogoro ndio pekee wenye ardhi inayostawi mazao yote ya chakula na ni miongoni mwa mikoa inayotegemewa kulisha Taifa hivyo lazima kuwe na mikakati ya pamoja ya kuhakikisha inazalisha chakula kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na ziada ya kulisha mikoa mingine.
No comments