CUF, Lipumba yaanza upya
Uongozi wa chama Cha Wananchi ( CUF), unaotambuliwa na msajili wa vyama vya siasa nchini, umeitambulisha rasmi bodi mpya ya wadhamini baada ya kupata usajili Juni 12, mwaka huu kutoka Wakala wa Ufilisi na Udhamini (Rita).
Kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa, inakitaka kila chama cha siasa kilichosajiliwa kuwa na bodi ya wadhamini iliyopata usajili Rita, ambayo itadumu kwa kipindi cha miaka mitano.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo, (Jumatano) Katibu Mkuu wa Bodi hiyo, Thomas Malima amesema baada ya usajili huo, Baraza Kuu la Uongozi chini ya Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba liliketi na kufanya uteuzi wa wajumbe tisa wa bodi hiyo baada ya kujiridhisha bodi iliyokuwapo imemaliza muda wake.
“Sasa chama kinarejea katika hali yake na kumaliza migogoro yote, baraza moja, kamati ya utendaji moja na Bodi ya wadhamini moja, tunatoa onyo kali na tutamchukulia hatua kali za kinidhamu mwanachama yeyote atakayesikika akitoa matamko yoyote yanayohusiana na chama asiyetambuliwa kikatiba,” amesema Malima.
Kadhalika Malima ametaja maazimio ya kikao cha bodi hiyo mpya kilichoketi Juni 17, mwaka huu na kusema bodi hiyo iliadhimia kufuta kesi zote zilizofunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini.
Mengine yaliyoadhimiwa ni kuziandikia benki zote zenye akaunti ya CUF zifungulie miamala yake na akaunti ya NMB tawi la Temeke iwe akaunti ya bodi ya wadhamini.
No comments