Wabunge wacharurana hifadhi maliasili
DODOMA Jumatatu22/5/2017
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
WABUNGE wamecharurana ndani ya Bunge baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata, kuwashutumu wabunge wenzake kuwa wanaingilia masuala ya kitaalamu hasa yanayohusu haki za hifadhi za taifa na wananchi.
Katika mchango wake wakati wa semina ya wabunge kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa maliasili, malikale na maendeleo ya utalii iliyofanyika mjini Dodoma, Mlata aliwataka wabunge wenzake kuacha tabia ya kuingilia masuala ya sekta ya maliasili na utalii. Katika semina hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na kufanyika jana, Mlata alisema wanasiasa wamekuwa wanawaingilia wataalam jambo linalosababisha wataalamu hao kushindwa kutekeleza sawia mipango yao katika uhifadhi na utalii.
Kutokana na hoja ya Mlata,Mbunge wa Chemba Juma Nkamia (CCM) aliomba kutoa taarifa na kumueleza mbunge huyo kuwa hakuna maendeleo yanayopatikana wala dunia inayoendeshwa bila wanasiasa. “Wanasiasa nao wana utalaamu wao kama wengi hawana shauri yao. Nalisema hivyo kwa sababu na huko nje inaenezwa hivi kimakosa kuwa wanasiasa wasiingilie wataalamu,” alisema Nkamia na kushangiliwa na wenzake.
Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalum Riziki Lulida (CUF) alimuunga mkono Mlata na kusisitiza kuwa ni kweli wapo baadhi ya wanasiasa kimakosa wamekuwa wakiingilia masuala ya utendaji ya Wizara hiyo. “Utakuta wapo wabunge wanatetea ng’ombe kuingia katika hifadhi za misitu. Mfano msitu wa Selous wanasiasa wamekuwa wanaingilia sana hali ambayo imefanya kuharibu njia za mapito za wanyama,” alisema Lulida.
Mbunge huyo alitolea mfano wa tembo walionekana katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kueleza kuwa wanyama hao hawakuwa na makosa kwa kuwa walikuwa wakifuata njia zao za asili, lakini tatizo liko kwa wananchi wanaojenga bila kufuata ushauri wa wataalamu na kutetewa na wanasiasa. Naye Mbunge wa Kilolo (CCM), Venance Mwamoto alitetea hoja ya wanasiasa kuingia masuala ya wataalamu na kufafanua kuwa wamekuwa wakifanya hivyo baada ya kuona mipango inayopangwa na wataalamu hao haitekelezwi inavyopaswa.
“Kuna umuhimu wa wataalamu kuhakikisha mipango wanaiyopanga wanaitekeleza ipasavyo, sisi wanasiasa lazima tuingilie pale tunapoona mambo hayaendi,” alisisitiza. Edward Mwalongo (Njombe Mjini-CCM) alisema lazima wanasiasa waingilie wanapoona wataalam wanatekeleza masuala mbalimbali kinyume na mipango iliyopangwa. Alitoa mfano ukitaka kukata miti lazima ulipie kibali na hivyo kuitaka Serikali kuondoa malipo hayo ili iwe motisha kwa wananchi wanaovuna maliasili yake.
Wabunge wengine waliochangia katika semina hiyo, waliitaka Serikali kuweka mipango mizuri itakayoondoa migogoro baina ya wananchi na maeneo ya hifadhi kwani vyote vina umuhimu katika taifa hilo. Awali akiwasilisha mada katika semina hiyo kuhusu sababu za kuhifadhi uoto wa asili na wanyamapori, Mkurugenziwa Wanyamapori Profesa Alexander Songorwa alisema uoto wa asili usipohifadhiwa, ipo hatari ya kupungua kwa maeneo yaliyohifadhi hewa ya oxygen.
Changamoto nyingine za kutohifadhi uoto wa asili ni kufa kwa mfumo wa ikolojia, wanyamapori na vivutio vya kitalii kuharibika na kupungua na hata kutoweka. Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Dos Santos Silayo, alisema wakati akiwasilisha mada ya umuhimu wa uhifadhi wa misitu nchini kuwa ni vema misitu ikatunzwa kwa kuwa ndio utajiri mkubwa kwa Watanzania. Alisema misitu ndio huzalisha vyanzo vya maji, husababisha mvua, hutumika kama utalii wa ikolojia, hutunza wanyama na ndege na pia husaidia katika kutunza mazingira.
No comments