Breaking News

UTEUZI WA MAKOCHA NDIO CHANZO CHA KUFANYA VIBAYA KWA KILIMANJARO STARS- JULIO

BAADA ya timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kufanya vibaya kwenye michuano ya Chalenji inayoendelea nchini Kenya, baadhi ya makocha nchini wametoa maoni yao kufuatia kuondolewa kwa timu hiyo.

Kilimanjaro Stars iliwasili nchini jana ikitokea Kenya ambapo katika michezo minne iliyocheza ilijikuta ikiambulia pointi moja baada ya kufungwa michezo mitatu na kutoka sare mchezo mmoja.

Kocha wa Dodoma FC, Jamhuri Kiwhelu ‘Julio’ alisema kufanya vibaya kwa Kilimanjaro Stars kumetokana na maandalizi duni pamoja na uteuzi wa kocha.

“Mimi niseme tu ukweli, Kilimanjaro Stars ilihitaji kocha ambaye anawajua wachezaji vizuri na anazijua vyema changamoto za soka letu, namuheshimu Ninje (kocha wa Kilimanjaro Stars), lakini hakuwa na jipya,” alisema Julio, alipokuwa akizungumza na kituo kimoja cha Radio.

Alisema kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), halikufanya chaguo sahihi kumpa timu Ninje ambaye alitumia michuano hiyo kuingiza mfumo mpya wa uchezaji.

“Wachezaji ni walewale, chini ya Salum Mayanga, timu ilikuwa inacheza, huwezi kuingiza mfumo mpya kwenye mashindano na matokeo yake ndio haya tumetia aibu,” alisema Julio.

Kwa upande wake, Kocha Abdallah Kibadeni, alisema wachezaji wa Kilimanjaro Stars wameshindwa kuona thamani ya kuvaa jezi za Taifa.

“Lakini pia ni lazima kujua changamoto za wachezaji, kufanya vibaya kwa Kilimnajaro Stars iwe chachu ya kujipanga upya na kuwa makini katika maandalizi ya michuano mingine,” alisema Kibadeni.

Naye nyota wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Ally Mayai, alisema kocha Ninje alifanya makosa kuanzisha staili mpya ya uchezaji wakati wa michuano hiyo.

“Inawezekana alikuwa na lengo zuri, lakini huwezi kutambulisha mfumo mpya wakati wa mashindano au siku chache kabla ya mashindano hili limetugharimu,” alisema Mayai.

Akiwasili nchini jana asubuhi pamoja na kikosi hicho, Kocha wa Kilimanjaro Stars, Ninje, mbali na kuomba radhi kwa Watanzania kutokana na kufanya vibaya kwenye michuano hiyo, alisema kuwa timu yake haikuwa na bahati kwenye michuano hiyo.

Aidha, alikiri mfumo mpya aliouanzisha kwenye kikosi cha timu hiyo umewagharimu, lakini akatetea kuwa kama utafanyiwa kazi utaifanya timu hiyo ya taifa kuwa moto.

No comments