MFUNGWA ALIYEKAA GEREZANI MIAKA 43 KISHA KUPEWA MSAMAHA NA RAIS MAGUFULI AFUNGUKA
Dar es Salaam. Rais John Magufuli alishangaza wengi alipotaja jina la mfungwa aitwaye Mganga Matonya, mwenye umri wa miaka 85, wakati akitangaza msamaha kwa watu 61 waliohukumiwa kunyongwa na mmoja aliyekuwa na kifungo cha maisha.
Haikuwa kitu cha kawaida kwa mkuu wa nchi kutaja jina la mfungwa, lakini ni mwendelezo wa maajabu yaliyowahi kumkuta Matonya katika maisha yake ya gerezani. Mara ya kwanza alifutiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.
“Namshukuru sana Rais Magufuli,” alisema Matonya alipoongea na mwandishi wetu jana akiwa kijijini kwake Wiliko mkoani Dodoma.
“Sikutegemea kama nitatoka gerezani. Naomba salamu zimfikie kwani sijui namna ya kuonana naye. Ningebahatika kuonana naye siku ile nilipotoka gerezani, ningemkumbatia kwa furaha.”
Matonya alipata taarifa za msamaha akiwa gereza la Kingolwira mkoani Morogoro, lakini awali alikuwa Gereza la Isanga mkoani Dodoma akiwa mahabusu baada ya kufanya kosa akiwa na umri wa miaka 39. Aliishi Isanga hadi Mei 10, 1980 wakati alipohukumiwa.
“Hakimu aliamuru ninyongwe mpaka kufa. Wakati nasubiri utekelezaji wa hatua hiyo mwaka 1984, rais wa wakati huo, Julius Nyerere alinibadilishia adhabu kutoka kunyongwa hadi kifungo cha maisha,” alisema Matonya.
Baada ya kuhukumiwa kunyongwa, Matonya na mwenzake walisubiri kifo kwa miaka mitano, lakini mabadiliko ya tabia waliyoonyesha wakiwa gerezani yalishawishi wasimamizi wao wapendekeze majina yao ili wabadilishiwe adhabu.
Baada ya Rais Nyerere kuwapunguzia adhabu hiyo, wawili hao walihamishwa kutoka Gereza la Isanga mkoani Dodoma na kwenda Kingolwira mkoani Morogoro.
Anasema hakuwahi kufikiria kuwa kuna siku angetoka gerezani, zaidi ya kujipa matumani na kumuomba Mwenyezi Mungu amnusuru na adhabu ya kufia ndani ya kuta za majengo hayo.
Jana ilikuwa siku ya furaha kwa Matonya, familia yake, ndugu na wanakijiji wa Wiliko, kijiji ambacho kiko takriban kilomita 85 kutoka Dodoma Mjini.
Akizungumza na Mwananchi jana, Matonya alionyesha furaha, mwenye kutafuta maneno asijue la kusema zaidi ya shukrani nyingi kwa Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kumsamehe adhabu ambayo ni nadra kunusurika isipokuwa kwa kushindana kisheria.
“Natamani kuonana na Rais Magufuli na kuongea naye mambo mbalimbali, lakini sina uwezo,” alisema Matonya.
“Lakini kupitia gazeti hili naamini ujumbe utamfikia. Kwa kweli, namshukuru sana kwa hili.”
Pamoja na Rais kumtaja jina, Matonya anasena hakuwa anafahamu lolote kuhusu msamaha huo.
“Taarifa zilinifikia ghafla,” alisema.
“Siku hiyo nilikuwa nimepumzika gerezani na wenzangu walikuwa wanaangalia televisheni. Mara nikasikia wenzangu wakiniita. ‘Mzee Matonya, Mzee Matonya. Njoo uone huku jina lako limetajwa na Rais Magufuli kuwa umeachiwa huru’.
“Sikuamini na sikula chakula kwa furaha niliyokuwa nayo.”
Kosa mpaka kufungwa
Matonya na mwenzake anayeitwa Myeya Nyagalo walikamatwa Oktoba 1974 wakati walipoenda kuuza ng’ombe wa wizi kwenye mnada katika Kijiji cha Nyang’oro kilichopo kati ya Iringa na Dodoma. Walikuwa wamemuua mwenye mifugo hiyo kwa mkuki wakati wakiiba na hivyo walikuwa wanasakwa hadi walipoibuka mnadani.
Matonya na Nyagalo walikuwa miongoni mwa watu 12 walioorodheshwa kuwa walihusika katika mauaji hayo.
Akikumbuka tukio hilo, Matonya alisema wakati huo alikuwa kijana na mwenye tabia ya wizi wa mifugo.
Anasema siku alipofanya kosa hilo, alikuwa na Nyagalo na vijana wengine wawili wa kabila la Kimasai walioshirikiana kuiba ng’ombe hao.
“Tuliandaa mpango wa kujiongezea mifugo. Baada ya kujiridhisha wapi tunaenda kuiba mifugo hiyo, tuliamua kwenda,” alisema Matonya.
“Haikuwa mara yetu ya kwanza. tulishafanya matukio kama hayo maeneo mengine. Lakini, kwa hili, arobaini za mwizi zilikuwa zimefika. Tulipata upinzani mkubwa uliosababisha mapigano na kifo cha mwenye mali.
“Mimi na mwenzangu Nyagalo hatukufahamu kama mtu yule amefariki. Tulijua tumemjeruhi tu.”
Alisema wenzao walifahamu kwamba mwenye mali hangepona. Alisema tofauti na matukio ya awali, wenzao walitaka wagawane mifugo waliyoiba na kila mmoja ashike njia zake.
“Tulishangaa, lakini mwisho wa siku tuligawana, tukaachana,” alisema.
Alisema baada ya muda hawakuwa na njia nyingine zaidi ya kupeleka mifugo mnadani kuiuza bila kujali kama Jeshi la Polisi lilikuwa linawatafuta. Ndio maana walikamatwa kirahisi.
Familia ya Matonya
Leo hii, Matonya amerejea mtaani ambako ana watoto sita, wajukuu 33 na vitukuu ambao idadi yake haikuweza kupatikana mara moja. Lakini alimuacha mkewe akiwa na watoto wawili na ujauzito wa miezi nane, hivyo watoto waliozaliwa wakati akiwa jela wanahesabika kuwa wake.
Kama ilivyokuwa kwa Nguza Mbangu Vicking na mwanae Papii Kocha waliotoka gerezani saa chache baada ya kutangaziwa msamaha, ndivyo ilivyokuwa kwa Matonya na mwenzake waliotoka gerezani juzi.
Mzee Matonya alisema anaangalia uwezekano wa kujikita kwenye kilimo, shughuli aliyokuwa akiifanya kabla ya kuhukumiwa, lakini anasema umri ushaenda.
Baada ya kuishi gerezani mwezi mmoja, alizaliwa mtoto ambaye mkewe alimuita Aron (45) ambaye akiwa shule ya msingi, alikuwa akipokea barua za baba yake kutoka kwa wafungwa waliokuwa wanamaliza kutumikia adhabu zao au mahabusu walioshinda kesi.
Aron ambaye kwa sasa ni baba wa watoto wanne na wajukuu, alisema alijisikia furaha baada ya kupata taarifa za kuachiwa kwa baba yake kwa kuwa hakuamini kama angekuwa huru tena.
“Tulikataa tamaa kama Mzee angetoka gerezani,” alisema Aron.
“Niliwahi kwenda kumuona mara nne na mwisho ilikuwa ni mwaka 2014. Ninapozungumza naye. Najisikia furaha iliyopitiliza. Kila mtu hapa kijijini haamini kilichotokea,” alisema Aron.
Baada ya kuongezeka kwa mzee wao, Aron anasema watu hawakauki nyumbani kwao kwa kuwa kila mtu anataka kumuona na kumshika mkono. Hapo nyumbani, anasema watu hawalali, wanashangilia huku wengine wakifanya maombi ya kumshukuru Mungu na Rais Magufuli aliyempa msahama.
No comments