LWANDAMINA AGEUKIA MICHUANO YA CAF
WAKATI klabu nyingine za Ligi Kuu Tanzania Bara zikiwa kwenye mchakato wa kuimarisha vikosi vyao kwa ajili ya ligi, Kocha wa Yanga, George Lwandamina, amesema usajili watakaoufanya ni kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Yanga itashiriki michuano hiyo mikubwa Afrika kwa ngazi ya klabu kuanzia Februari mwakani.
Kikosi hicho cha Yanga kinampango wa kusajili wachezaji watatu kwenye safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji.Akizungumza jijini Dar es Salaam, Lwandamina, alisema kwa sasa ni wakati wa kujipanga kwa ajili ya michuano ya kimataifa.
“Nina kikosi kizuri, lakini kwa michuano ya kimataifa ni lazima tuongeze wachezaji kwa ajili kupambana kwenye michuano hiyo, tunataka kuona tunafanya vizuri,” alisema Lwandamina.
Lwandamina, alisema kuwa yapo mapendekezo aliyoyawakilisha kwa uongozi wa timu hiyo ambapo ameeleza wachezaji wanaopaswa kuongezwa kwenye kikosi chake.
“Najua uongozi unafanyia kazi ripoti yangu, ni lazima pia kuangalia michuano ya kimataifa na ukiangalia tumebakiza Januari tu kabla ya kuanza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Lwandamina.
Aidha, Lwandamina, alisema katika ripoti hiyo ameelezea pia ni wachezaji gani ambao uongozi haupaswi kuwaachia waondoke.
Kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Uhuru kujianda na michezo ya Ligi Kuu ambapo mchezo unaofuata watacheza na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
No comments