Breaking News

IDARA YA UHAMIAJI YAMUHOJI ASKOFU WA KATOLIKI KUHUSU URAIA WAKE

Askofu Severine Niwemugizi.

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Rulenge, Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, Severine Niwemugizi (61), amehojiwa na Idara ya Uhamiaji kuhusiana na uraia wake. Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Askofu Niwemugizi alisema mara ya kwanza alihojiwa Novemba 28 mwaka huu na mara ya pili alihojiwa Desemba 4, mwaka huu.

“Mara ya kwanza niliitwa na kufika ofisi za uhamiaji Ngara, Novemba 28 na mara ya pili niliitwa Desemba 4.

“Niliombwa kibali kinachoniruhusu kuwa nchini, nikashangaa, nikasema mimi ni Mtanzania, nikaambiwa nilete document (nyaraka).

“Nilipeleka hati ya kusafiria, kitambulisho cha kupigia kura na cheti cha kuzaliwa, wakasema wataniita tena.

“Baada ya kuitwa mara ya pili, nilipewa fomu ya kujaza ambayo bado naendelea kuijaza hadi sasa.

“Waliniita tena wakasema bado wanataka kujiridhisha ndio maana wanataka nijaze fomu,
ninaendelea kuifanyia kazi mpaka nitakapokuwa nimeikamilisha yote,” alisema Askofu Niwemugizi ambaye amewahi kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC).

Mahojiano kati yake na Mwandishi wa Mtanzania yalikuwa hivi.

Swali: Je, ulizaliwa wapi?

Jibu: Nilizaliwa katika Kitongoji cha Kayanza, Kijiji cha Kabukome, Kata ya Nyarubungo, Wilaya ya Biharamulo.

Swali: Ulizaliwa tarehe ngapi?

Jibu: Nilizaliwa Juni 3, mwaka 1956.

Swali: Ulibatizwa wapi?

Jibu: Nilibatizwa katika Parokia ya Katoke, Biharamulo.

Swali: Elimu ya Msingi na Sekondari ulisoma wapi?

Jibu: Nilisoma Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo na Shule ya Sekondari Nyakato Bukoba (O-level).

Baada ya kumaliza ‘O-level’ niliingia Seminari Kuu ya Ntungamo Bukoba halafu nikatoka hapo nikaenda Kipalapala Tabora.

Swali: Wazazi wako walizaliwa wapi?

Jibu: Walizaliwa sehemu mbalimbali, mama alizaliwa Lusahunga na baba alizaliwa katika Tarafa ya Nyarubungo, Kijiji cha Kabukome Kitongoji cha Kayanza.

Swali: Katika maisha yako yote je, ulishawahi kuhisiwa kuhusu uraia wako?

Jibu: Sijawahi kuulizwa, muda wote nimetumia passport (hati ya kusafiria) ya Tanzania na hakuna aliyewahi kuniuliza suala la uraia.

Swali: Je, unafikiri kwanini hili linajitokeza sasa?

Jibu: Baada ya hivi karibuni kutoa ushauri, kwamba ni vizuri mchakato wa Katiba ukarejewa, watu wali-react, sasa naweza kupata picha nini kimesababisha nianze kuhojiwa.

Swali: Je, Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC) wana taarifa kwamba umeitwa uhamiaji?
Jibu: Sijawataarifu kwa sababu suala hili lilionekana bado liko chini chini, lakini nafikiri nitatafuta namna ya kuwafahamisha juu ya jambo hili.

Swali: Je, mbali na kuwa Askofu, uliwahi kushika nafasi gani katika Kanisa Katoliki?

Jibu: Niliwahi kuwa Rais wa TEC, kuanzia mwaka 2000 hadi 2006 na baadaye nikawa Mkamu wa Rais kuanzia mwaka 2012 hadi 2015.

Swali: Je, una hofu yoyote juu ya usalama wako?

Jibu: Mimi sina hofu na usalama kwa sababu ninajua kufa ni mara moja. Kwa hiyo, ninabaki kivulini, ninazungumza tu ninavyowajibika kama askofu.

UHAMIAJI

MTANZANIA lilizungumza na Msemaji Mkuu Idara ya Uhamiaji, Mrakibu Ally Mtanda, ambaye alikiri askofu huyo kuhojiwa.

“Ni kweli anahojiwa na ofisi yetu ya Wilaya ya Ngara, ni suala tu la tuhuma si kwamba ni kweli au la, hivyo itakapothibitika basi itajulikana,” alisema Mtanda.

No comments