Breaking News

OFISA MTENDAJI MKUU NMG KUJIUZULU

  Dar es Salaam. Bodi ya kampuni ya Nation Media Group (NMG) imetangaza kujiuzulu kwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Joseph Muganda kuanzia Januari 31, 2018.

Taarifa iliyotolewa jana na mwenyekiti wa Bodi ya NMG, Wilfred Kiboro inaeleza kuwa kutokana na kuondoka kwake, Mkurugenzi wa Fedha wa NMG, Stephen Gitagama atakaimu nafasi hiyo wakati bodi ikitafuta mtu atakayemrithi Muganda.

Muganda alijiunga na NMG Julai, 2015 na amefanikiwa kuongoza mkakati wa kuifanya kampuni ikue vizuri katika safari mpya ya kidigitali.

“Muganda ameongoza kwa ujasiri kutathmini biashara ya bidhaa zetu, ameongoza kufanya mageuzi ya kimfumo na kuielekeza tena kampuni katika kutumia fursa zilizojitokeza kutokana na mitandao ya jamii kuvuruga sekta ya habari,” anasema Kiboro katika taarifa yake.

“Ataiacha kampuni ikiwa inawaelewa wateja na iliyobadilika kwa haraka na ambayo mafanikio yake kibiashara tayari ni dhahiri kwa kuangalia matarajio ya faida kutokana na uwekezaji katika mikakati ya kidigitali. Tunamtakia mafanikio katika mipango yake ya baadaye.”

Kiboro amewahakikishia wanahisa na wadau wote wa NMG na umma kwamba kwamba kipindi cha mpito cha mabadiliko ya uongozi hakitakuwa na matatizo na kitafanyika kwa haraka.

NMG, ambayo inamilikiwa na umma, ni kampuni yenye mafanikio makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na inajivunia mafanikio ya kidigitali, ikiwa na watu milioni 30 wanaotembelea kurasa zake.

NMG inachapisha magazeti ya Nation na Taifa Leo nchini Kenya, The EastAfrican ambalo ni la kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Daily Monitor la Uganda, na Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti ya Tanzania na pia matoleo ya kielektroniki.

Pia inamiliki vituo vya televisheni vya NTV Kenya, na NTV na Spark pamoja na vituo vya redio vya KFM na Dembe nchini Uganda. Pia inamiliki kituo cha redio cha Nation FM cha Kenya.

NMG imejisajili katika masoko ya hisa ya Kampala, Dar es Salaam na Kigali. 

No comments