Breaking News

Nyalandu, Mbowe kumnadi mgombea wa Chadema

Aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu leo  ataungana na viongozi wa Chadema kwenye kampeni za  uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika katika kata 43 nchi.

 Akizungumza jana Novemba 11, kwenye ufunguzi wa kampeni hizo Kimara Suka jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema Freeman  Mbowe alisema  amempokea Nyalandu na ataungana naye kwenye mkutano mwingine kama huo utakaofanyika Mtwara mjini leo.

‘’Kila anayeondoka chama tawala anaitwa fisadi, potelea mbali wamempokea na wengine wengi watahamia kuleta mabadiliko’’ alisema na kuongeza

"Mabadiliko hayaji  ghafla  yanakuja taratibu na ujio wao ndiyo mwanzo wa mabadiliko  tulipoanza na tulipo sasa kuna tofauti kubwa" amesema  Mbowe.

Alifafanua  kwamba haungi mkono nchi kuwa na wezi, lakini anashauri sheria iachwe iamue haki badala ya kuingiliwa kama inavyofanyika kwa mahakama.Huku akidai kwamba watawala wana hofu ndiyo maana hawataki ushauri.

Alisema wataendelea kupigania haki ya kupigania haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na ipo siku wataingia mtaani kuidai bila kuogopa vifaru.

Alisema huu siyo wakati wa kuogopa na kukaa kimya ni wakati wa kusimama na kutetea haki ya kufanya siasa.

Kuhusu uchumi kusinyaa alisema ni kweli umesinyaa na inaonekana wazi jinsi maisha yalivyo  wananchi, wafanyabiashara, watawala wote wanalia njaa hakuna mwenye nafuu.

Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob alisema anahitaji kuongeza nguvu ya kuleta maendeleo katika manispaa hiyo, hivyo  mgombea udiwani  kata ya Saranga Ephram Kinyafu anatosha.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani Frederick Sumaye alihoji kuhusu hali za wananchi kuendelea kuwa mbaya.

"Tumeamua na tunamaanisha wakati huu ushindi ni lazima, na mtakaotupa ushindi ni nyie wananchi" alisema Sumaye.

No comments