Breaking News

Mahakama yasitisha uchaguzi Liberia

Hii ina maana kwamba uchaguzi wa marudio utapangiowa tarehe nyingine baada ya suala zima kukamilika na ikiwa LP itashindwa. 
Lakini ikiwa itashinda utaitishwa uchaguzi mpya. Hali hii inaweza kusababisha kuundwa kwa serikali ya muda ambapo baadhi ya watu wanapendekeza muhula wa Sirleaf uendelee hadi Januari 18.

Monrovia, Liberia. Mahakama ya Juu ya Liberia imeiamuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha maandalizi yoyote yanayohusiana na uchaguzi wa marudio wa urais uliopangwa Novemba 7 baada ya kusikiliza maombi yaliyowasilishwa na chama cha upinzani cha Liberty (LP).

Chama hicho kilifungua kesi Mahakama ya Juu kikiomba kusitishwa kwa uchaguzi huo wa marudio kwa maelezo ule wa Oktoba 10 uliohusu rais na wabunge uligubikwa na dosari na udanganyifu.

Chama tawala cha Unity Party, na vya upinzani vya All Liberian Party na Alternative National Congress vilijiunga na LP katika kupinga marudio.

Mwanasoka wa zamani na Seneta wa kaunti ya Montserrado, George Weah wa Muungano wa Mabadiliko ya Demokrasia (CDC) alikuwa anaongoza baada ya kujikingia asilimia 38 ya kura huku makamu wa rais wa Liberia, Joseph Boakai wa Unity Party alishika nafasi ya pili akiwa na asilimia 28.

Kutokana na wagombea wawili hao kushika nafasi mbili za juu ndio wanatarajiwa kuumana Jumanne ijayo ili kumpata mshindi wa kurithi kiti cha urais kinachoachwa na Rais Ellen Johnson Sirleaf, mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia barani Afrika.

Jaji Mkuu Francis Korkpor pamoja na majaji wengine walikataa katakata kuzungumza jana jioni kuhusu uamuzi uliofikiwa, lakini Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Mahakama ya Juu, Ambrose Nmah, alisema jopo hilo halikutoka na uamuzi wowote.

"Hakuna uamuzi uliofikiwa: kama mnavyofahamu kwamba majaji hawakuwepo nchini, wamerejea leo na wamekuja moja kwa moja kutoka uwanja wa ndege kwa ajili ya kupata maelezo mafupi kuhusu kesi hii," alisema.

Waandishi wa habari wa gazeti la Front Page Africa walimshuhudia jaji mkuu akishuka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Roberts na moja kwa moja alikwenda ofisini ambako yeye na majaji wenzake walijifungia wakijadili ombi linalowataka watoe amri ya kuzuia uchaguzi wa marudio wa Novemba 7.

Hata hivyo, chanzo kimoja cha kuaminika kimeliambia gazeti hili kwamba Mahakama ya Juu, Jumanne jioni ilitoa amri ya kusitisha uchaguzi kama ilivyoombwa na chama cha LP ikiwa na maana uchaguzi wa marudio uliokuwa umepangwa kufanyika Jumanne ijayo sasa hautafanyika hadi kesi hiyo itakapokamilika kusikilizwa pamoja na rufani yake.

"Hii ina maana kwamba uchaguzi wa marudio utapangiowa tarehe nyingine baada ya suala zima kukamilika na ikiwa LP itashindwa. Lakini ikiwa itashinda utaitishwa uchaguzi mpya. Hali hii inaweza kusababisha kuundwa kwa serikali ya muda ambapo baadhi ya watu wanapendekeza muhula wa Sirleaf uendelee hadi Januari 18,” chanzo hicho kimesema.

No comments