Breaking News

KIVUMBI CHA UCHAGUZI KUHAMIA JIMBO LA NYALANDU

Uchaguzi mdogo wa ubunge kufanyika nchini ulikuwa katika jimbo la Dimani baada ya mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Tahiri Ally kufariki dunia Novemba 11 mwaka jana na uchaguzi kufanyika Januari ambapo mshindi alikuwa Juma Ali Juma wa CCM.

Kivumbi cha uchaguzi mdogo wa ubunge kitahamia katika jimbo la Singida Kaskazini baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhusu jimbo hilo kuwa wazi na linaweza kuitisha uchaguzi.

Uchaguzi mdogo wa ubunge kufanyika nchini ulikuwa katika jimbo la Dimani baada ya mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Tahiri Ally kufariki dunia Novemba 11 mwaka jana na uchaguzi kufanyika Januari ambapo mshindi alikuwa Juma Ali Juma wa CCM.

Kwa jimbo la Singida Kaskazini uamuzi wa Spika Ndugai kutangaza jimbo hilo kuwa wazi umetokana na aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Lazaro Nyalandu kutangaza kujiuzulu mwanzoni mwa wiki hii kwa kumwandikia barua kiongozi huyo wa Bunge juu ya hatua hiyo.

Hata hivyo, kumekuwa mvutano kuhusu nani aliyeanza kuchukua hatua kati ya CCM na Nyalandu kwani taarifa ya jana na ile ya Novemba 1 ya Spika zimekuwa zikieleza Nyalandu alichukuliwa hatua na chama chake lakini haielezi kama imepokea barua yake ya kujizulu ambayo aliiandikia Bunge.

Hatua ya Nyalandu kujiuzulu inatoa fursa kwa vyama vya siasa hususan CCM, Chadema, CUF na ACT- Wazalendo na vingine kuingia katika ulingo kuchuana kuwania jimbo hilo huku tayari baadhi ya vyama vikieleza viko tayari ila vinasubiri NEC itangaze mchakato.

Vyama hivyo vimetoa kauli hiyo muda mfupi baada ya taarifa ya ofisi ya Bunge iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari Elimu kwa Umma na Mawasiliano iliyoeleza Spika Ndugai kumjulisha Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage kuwa jimbo la Singida Kaskazini liko wazi.

Kivumbi hicho kinatokana na tetesi huenda Nyalandu akarejea tena kutetea jimbo hilo akikiwakilisha Chadema huku CCM ikitaka kubaki nalo jambo ambalo wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaona utakuwa mpambano mkali.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima alipotafutwa kujua kama amepokea barua na lini mchakato wa uchaguzi utaanza, alijibu kwa ujumbe mfupi wa maandishi ‘mtajulishwa.’

Katika taarifa ya Bunge ilisema jimbo hilo limekuwa wazi baada ya aliyekuwa mbunge wake Lazaro Nyalandu kufutwa uanachama na Chama cha Mapinduzi (CCM), Oktoba 30.

“Kufuatia barua hiyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi, inaweza kuendelea na mchakato wa kumpata mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi ya jimbo la Singida Kaskazini,” ilieleza taarifa hiyo

Spika aliandika barua hiyo kwa mujibu wa kifungu 37(3) cha Sheria ya NEC (Sura ya 343, ya mwaka 2015) kinachoelekeza pale ambapo mbunge, atajiuzulu, atakufa au sababu nyingine yoyote tofauti na zilizoainishwa katika kifungu cha 113, Spika atamjulisha Mwenyekiti wa NEC na kutangaza kwenye Gazeti la Serikali kwamba kiti hicho cha ubunge kiko wazi.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji alisema “sisi tuko tayari kwa uchaguzi, tunachokisubiri ni tangazo tu la Tume ya Uchaguzi ili tuanze ‘procedure’ za ndani ya chama lakini uhindi kwa jimbo hilo ni lazima na wanachama wasubiri kuona ushindi.”

Mwananchi lilipotaka kujua endapo Nyalandu atapitishwa kutetea jimbo hilo, Dk Mashinji alisema “hilo ni suala la kidemokrasia, kama atapitishwa sawa na kama hatapitishwa sawa kwani ni ‘process’ za ndani ya chama.”

Naibu Katibu Mkuu wa CCM- Bara, Rodrick Mpogolo alipoulizwa kuhusu mchakato huo alisema “hilo mtafute Katibu Mkuu (Abdulrahman Kinana).” Alipoelezwa hapatikani akadai atafutwe Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ambaye simu zake za kiganjani zilikuwa zikiita bila kupokelewa.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Habari CUF upande wa mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, Abdul Kambaya alisema wanasubiri Tume itangaze mchakato ndipo wataamua.

“Lengo la chama chochote ni kushika dola na ili ushike dola unaanza huku chini, serikali za mitaa, kata na jimbo na mathalani Tume yenyewe haijatangaza mchakato hatujaamua ila dhamira ipo ni nani na tutashiriki vipi tusubiri,” alisema Kambaya

No comments